HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 10, 2019

HALOTEL YATOA MSAADA WA MADAWATI 55-KONDOA

  Naibu Waziri wa wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji, Mkurugenzi wa Kampuni ya Halotel Nguyen Van Son, ( katikati) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya hafla fupi ya kukabidhi madawati kwa ajili ya shule za Sekondari za wilaya ya Kondoa ikiwa ni moja ya malengo yake ya kuunga  mkono juhudi za wilaya hiyo pamoja nao, Wa kwanza Kushoto ni Mwenyekiti  wa CCm wilaya ya Kondoa Othman Gola. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kondoa Mustapha Semwiko,wa pili Makamu Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kondoa Hija Sulu.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akikabidhiwa madawati 55 na Mkurugenzi wa Kampuni ya Halotel Nguyen Van Son, kwa ajili ya shule za Sekondari za wilaya ya Kondoa ikiwa ni moja ya malengo yake ya kuunga  mkono juhudi za wilaya hiyo na Serikali  katika kuboresha elimu katika wilaya hiyo.

 NA MWANDISHI WETU

Kampuni ya simu za mikononi ya Halotel imetoa msaada wa madawati 55 kwa ajili ya Shule za Sekondari za Wilaya ya Kondoa ikiwa ni malengo yake ya kuunga mkono juhudi za wilaya hiyo na Serikali  katika kuboresha elimu.
Akipokea msaada huo wilayani humo juzi, Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji mbali na kuipongeza Halotel kwa msaada huo alisema madawati hayo ni msaada mkubwa kwa wilaya hiyo iliyojipambanua katika mkakati wa kipekee wa kukuza elimu.
Alisema Halmshauri hiyo na wanakondoa wote kwa ujumla wanatambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na kampuni hiyo ya simu katika kuboresha maisha ya wananchi hayo ikiwemo ya kuwaunganisha na nchi nzima kupitia njia ya mawasiliano ya simu za mkononi.
Dkt Kijaji alisema kupokelewa kwa madawati hayo kwa kiasi kikubwa kutasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati uliomo katika wilaya hiyo na hivyo kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kutokana na uhitaji uliopo kwa sasa.
“Naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza Halotel kwa msaada huu ikiwa kama mdau mkubwa wa maendeleo ya elimu ndani ya wilaya hii na Tanzania kwa ujumla, nitoe wito kwa taasisi  na kampuni zingine kuiga mfano huu kwa ajili ya maendeleo ya elimu katika Taifa letu” alisema Dk Kijaji
Aidha aliiomba Kampuni hiyo kuisaidia wilaya hiyo kuboresha elimu kwa kuwajengea maabara  itakayokuwa imeunganishwa na mfumo wa mtandao wa intaneti kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo masomo mbalimbali hususani ya sayansi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel Nguyen van Son, alisema kampuni hiyo kama mdau mkubwa maendeleo inayo mikakati mbalimbali katika kuboresha ya sekta ya elimu na afya nchini ikiwa ni mipango yake ya kushirikiana na Serikali kutatua changamoto mbalimbali zilizopo nchini.
Alisema kwa kutambua changamoto za kielimu zilizopo katika wilaya hiyo, Halotel iliona ina kila sababu ya kutoa msaada wa c madawati hayo kwa lengo la kumuunga mkono juhuzi za wilaya hiyo za kuboresha elimu zinazofanywa na Naibu Waziri wa Wizara ya fedha na Mipango  na Mbunge wa Jimbo hilo la Kondoa  Dk Ashatu Kijaji.
Alisema Halotel imekuwa ikiunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuboresha maisha ya wananchi wake kwa kushiriki katika mambo mbalimbali hususani katika sekta za afya na elimu, na hivyo kupunguza changamoto hizo zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitolea mfano katika sekta ya afya, Van Son alisema katika siku za hivi karibuni Halotel imenzisha mpango maalumu utakaowawezesha watu wenye matatizo ya kiafya kukutana na kupata ushauri wa tiba na matibabu kwa kuwaunganisha na madaktari bingwa chini ya mpango maalumu ulioanzishwa na kampuni hiyo.
Alisema Halotel inatambua changamoto zilizopo katika eneo hilo hivyo wao kama wadau wakubwa wa maendeleo wanaona wana kila sababu kushirikiana na Serikali katika kuzitatua na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo nchini inayofanywa chini ya uongozi wa awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli.
Naye Afisa elimu wa Wilaya ya Kondoa Hildegard Segunda alisema wilaya hiyo inakabiliwa na upungufu wa madawati 906 uliotokana na ongezeko la wanafunzi katika shule za Sekondari zilizopo katika wilaya hiyo.
Alisema hatua hiyo imetokana na muitiko wa wanafunzi kuingia shuleni kwa wingi na hususani baada ya kuondolewa gharama za  malipo chini ya mpango bure wa elimu uliotolewa na Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Pages