Na Mwandishi Wetu
RAIS Dkt. John Pombe
Magufuli amewataka Watanzania kuacha kulalamika na badala yake imewataka wananchi
wa mikoa ya kusini kutambua kuwa Serikali itaendelea kuwatumia na kuwaletea
maendeleo katika sekta za kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya
barabara.
Akizungumza katika hafla
ya uzinduzi wa barabara ya Tunduru-Nakapanya-Mangaka- Mtambaswala yenye urefu
wa kilometa 202.5, Rais Magufuli alisema Serikali yake itaendelea kuwajibika na
kusimamia miradi ya maendeleo inayobeba manufaa kwa Watanzania walio wengi.
Alisema kuwa Wananchi
wa mikoa ya Kusini wanapaswa kutambua historia ya ujenzi wa barabara hiyo
ulianzia katika Serikali za Awamu zilizopita ambapo kulikabiliwa na changamoto
mbalimbali wakati wa kuomba fedha kutoka wafadhili na wadau wa maendeleo.
Aidha Rais Magufuli
aliwataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kuiunga mkono Serikali katika
juhudi mbalimbali inazofanya za kuimarisha miundombinu ya barabara katika
ukanda wa kusini ikiwemo Mtwara kwani hapo awali hali ya miundombinu hiyo
haikuwa ya kuridhisha ukilinganisha na ilivyo sasa.
‘Mtakumbuka kuwa wakati
tulipokuwa tukiomba fedha za ujenzi wa daraja la Umoja lilnalounganisha
Tanzania na Msumbiji ambalo ndio kiungo muhimu baina ya mataifa haya, wafadhili
wote walikataa kutoa fedha kwani daraja hili linaingia porini katika kila nchi,
lakini tulisimama imara na kujenga daraja hili’ alisema Rais Magufuli.
Alisema kutokana na Mkoa
wa Mtwara kuwa katika ukanda muhimu katika usafirishaji wa bidhaa muhimu za kiuchumi
kupitia bandari, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Japan (JICA)
na Benki ya Mandeleo ya Afrika (AfDB) zilikubaliana kujenga barabara hiyo
ambayo kwa sasa itakuwa imefungua fursa za ukanda wa kiuchumi kwa kushirikiana
na nchi ya Msumbiji.
‘Ukitazama fedha hizi, si ndogo kwa mfano
kipande cha Tunduru-Nakapanya-Mangaka yenye urefu wa kilometa 137 kimetumia
wakandarasi watatu na washauri 3 na jumla ya Tsh Bilioni 182 zimetumika, na kipande
cha Mangaka- Mtambaswala chenye urefu wa kilometa 56 pia kiasi cha Tsh Biloioni
56 kimetumika’ alisema Rais Magufuli.
Alisema kuwa kitendo
cha wadau hao wa maendeleo kuiunga mkono Tanzania kinatokana na imani waliyonayo
kwa Serikali ya Awamu ya Tano, kwani yapo mataifa mbalimbali ya Bara la Afrika
yanayohitaji kujengewa barabara na kupatiwa misaada mbalimbali ya kijamii na
kiuchumi.
Kuhusu Kipande cha
barabara ya Masasi-Mtwara chenye urefu wa kilometa 150, Rais Magufuli
amewaagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Waziri wa Fedha na
Mipango kuandika barua ya mchanganuo wa maombi ya fedha kwa Shirika la Maendeleo
ya Japan (JICA) NA Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuanza mara moja ujenzi wa
barabara hiyo.
Kwa upande wake Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema kukamilika kwa
ujenzi wa barabara hiyo kumeweza kutimiza malengo ya Serikali ya kuiunganisha
ushoroba wa kusini katika kiwango cha lami.
Aliongeza kuwa katika
ujenzi huo, Shirika la Maendeleo ya Japan ilichangia asilimia 32.83, Benki ya
Maendeleo ya Afrika 64.79 na Serikali ya Tanzania ilitoa asilimia 2.38 ikiwemo
malipo ya fidia kwa wananchi pamoja na kodi.
Naye Mwakilishi Mkazi
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Alex Mubiru alisema kufunguliwa kwa
barabara hiyo kumeweza kutimiza ndoto ya waasisi wa Mataifa ya Tanzania na
Msumbiji Samora Machel na Julius Nyerere, ambapo walitaka mataifa hayo kuweza
kuunganisha na Daraja la Umoja ambalo kwa sasa litatoa fursa kwa wananchi wote kuweza
kuimarisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
No comments:
Post a Comment