Mkurugenzi wa
Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe
akifafanua umuhimu wa Kamati za Usimamizi wa Maafa wakati wa Mafunzo ya
Usimamizi wa Maafa mjini Musoma, tarehe 18 Aprili, 2019, Mafunzo hayo yaliratibiwa
na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa shughuli za maafa.
Na. OWM, MUSOMA
Wajumbe wa
Kamati ya Usimamizi wa Maafa Mkoani Mara wameiomba ofisi ya Waziri Mkuu, Idara
ya Uratibu wa maafa kuwajengea uwezo wa
kuunda kamati za Usimamizi wa Maafa mkoani humo. Wajumbe hao
wamebainisha kuwa wanataka kamati hizo ziundwe kuanzia ngazi ya kijiji hadi
ngazi ya mkoa ili mkoa huo uwe na uwezo wa kujiandaa, kuzuia, kukabili na kurejesha
hali kama maafa yatatokea.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015,
inaainisha majukumu ya kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi
ya Kijiji hadi mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni
kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika, pamoja
na Kuratibu na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za
dharura ndani ya Kijiji wilaya au mkoa. Pia kutoa taarifa za tahadhari
ndani ya eneo husika, hivyo kila mkoa hauna budi kuwa na kamati hizi.
Akiongea
wakati
akifungua mafunzo ya Usimamizi wa Maafa mjini Musoma, tarehe 18 Aprili,
2019, Mkuu
wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amesema kuwa yeye na wajumbe wa Kamati ya
Usimamizi wa Maafa ya mkoa wameamua kushirikiana na Ofisi ya Waziri
Mkuu Idara ya Uratibu Maafa, ili wawejengee uwezo utakao wawezesha kuanzisha kamati hizo kuanzia ngazi ya Kijiji, ili Kamati ya Usimamizi wa Maafa ya mkoa ambayo ilianzishwa rasmi kisheria kwa ajili ya kumshauri Mkuu wa mkoa masuala ya Usimamizi wa
maafa iweze kumshauri kwa weledi na kwa wakati.
“Ofisi ya
Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu Maafa ikishatujengea uwezo sisi jukumu letu ni
moja tu, ni kuhakiksha tunajiimarisha juu ya usimamizi wa maafa kuanzia ngazi
ya kijiji ili haya majanga ya Upepo mkali, Ukame, Ajali za vyombo vya usafiri
wa majini na nchi kavu, moto, Uharibifu wa mazao unaofanywa na tembo, tuwe na
uwezo wa kuyazuia au kupunguza madhara yake pindi yanapotokea mkoani hapa na hatutapata vifo, uharibu wa
mali na ulemavu wa kudumu kwa wananchi” Amesisitiza Malima.
Naye, Mkurugenzi
wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, amefafanua
kuwa ili kamati hizo ziwe na ufanisi katika usimamizi wa shughuli za maafa
zinapaswa kuandaa Mkakati wa Kupunguza madhara ya maafa pamoja na Mpango wa kujiandaa na
kukabili maafa.
“Ofisi ya
waziri Mkuu tutaendelea kuendesha mafunzo haya ili kuzijengea uwezo kamati hizi ambazo ni
chombo cha kisheria hapa nchini kwa ajili ya kutathimini na kutekeleza masuala
ya kitaalam kuhusu usimamizi wa maafa, kuzuia na kupunguza madhara ya majanga
ya aina zote katika mkoa lakini mkishapata mafunzo haya hakikisheni mnaweka
masuala y amaafakatika mipango yenu ya maendeleo.”
Mafunzo hayo
yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa shughuli za maafa,
yamehudhuriwa na wajumbe wote wa Kamati ya Usimamizi wa maafa wa mkoa pamoja kwa kuzingatia Kifungu cha 13 cha sheria ya
Usimamizi wa Maafa Na. 7 ya mwaka 2015, pamoja na baadhi ya wananchi wa kawaida walioalikwa katika kikao mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment