Mchoraji kutoka Tingatinga Arts, Agnes Mpate alkimuonyesha picha ya
kuchora Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Albert Jonkergouw
wakati wa Kongamano la wafanyabiashara Business Club Ilala lililofanyika
leo jijini Dar es Salaa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Albert Jonkergouw
akiangalia moja ya bidhaa za Mkurugenzi wa Malaika Home essentials,
Rachael Moyo wakati wa Kongamano la wafanyabiashara Business Club Ilala
lililofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha
biashara, Donatus Richard.
NA MWANDISHI WETU
KATIKA kuwaongeza uelewa, maarifa na
elimu ya kujenga nidhamu ya fedha kwenye biashara zao, Benki ya NMB imeahidi
kuwapeleka China kwa masomo na warsha wafanyabiashara 10 kutoka katika Klabu za
Biashara za benki hiyo ‘NMB Business Club,’ baadaye mwaka huu.
Ahadi hiyo imetolewa jana
jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa NMB, Donatus Richard,
wakati wa kongamano la Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati (MSE), wanaounda Klabu
za Biashara za NMB, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kardinali Rugambwa, Oysterbay.
Richard alibainisha kuwa,
lengo la ziara hiyo ya mafunzo ni kuimarisha uelewa wa masuala ya fedha
miongoni mwa wafanyabiashara wanaounda klabu hizo, lengo likiwa ni kuwaongezea
elimu ya kuhakikisha mtiririko wa fedha kwenye biashara zao, unakuwa mnyoofu.
Akisisitiza ahadi hiyo,
mbele ya wafanyabiashara zaidi ya 300 walioshiriki kongamano hilo, Richard
alisema kuwa mchakato wa namna ya kuwapata wateule wa ziara hiyo utatangazwa
miongoni mwao,ili kwenda kupata fursa za kimataifa, safari ikitarajiwa kufanywa
Oktoba mwaka huu.
“Ushindani kibiashara nchini
umekuwa mkubwa, nasi ndio maana tunatumia klabu hizi kufundisha mifumo, njia na
mipango rafiki ya kuimarisha biashara za wateja wetu hawa ambao pia ni mabalozi
wetu kwa jamii. Tutawapeleka China kujiongezea maarifa juu ya hilo,” alisema
Richard.
Awali akifungua kongamano
hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Albert Jonkergouw, alisema watayafanyia
kazi mapendekezo yote yatakayotolewa na wafanyabiashara wanaohudhuria
makongamano yao kutoka klabu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na punguzo la gharama
za uendeshaji wa akaunti ya biashara.
Jonkergouw alibainisha ya
kwamba, Klabu za Wafanyabiashara ni nzuri na muhimu sio tu kwa wanachama wake
na Benki ya NMB, bali pia kwa ustawi na ukuaji wa uchumi wa Taifa na kwamba
wafanyabiashara hao ni kati ya mabalozi wema wa benki hiyo.
“Kongamano hili ni kati ya
fursa tunazozitumia kusikiliza changamoto zenu, kujadiliana namna ya kuzitatua
na mwisho wa mwezi kwenda pamoja katika kasi ya uchumi wa mteja mmoja mmoja,
benki kama taasisi na taifa kwa ujumla wake,” alisisitiza Jonkergouw.
Akizungumza kwa niaba ya
wafanyabiashara waliohudhuria, aliishukuru NMB kwa kuwakabidhi baadhi yao vyeti
vya ubalozi mwema wa benki kwa wafanyabiashara wa kupigiwa mfano, Award
Mpandila, aliitaka Serikali kuwasaidia ujenga mazingira rafiki ya kibiashara.
Mpandila alifafanua kwamba,
moja ya changamoto zinazokwaza biashara zao ni tozo zisizo wazi hususani
bandarini, ambazo zinawakwamisha na kusababisha kutorejesha mikopo yao kwa
wakati, kutokana na kuchelewesha kwa uondoshaji mizigo bandarini.
No comments:
Post a Comment