Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
* Asema si jukumu lake kwa
mujibu wa Katiba ya Tanzania
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiwezi kusimamia Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa kama ambavyo imependekezwa na baadhi ya Wabunge.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 9,
2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya
bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka
2019/2020.
Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa
kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usisimamiwe na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na
badala yake usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Pia waliitaka Serikali
ishughulikie jambo hilo mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea.
Akitoa
ufafanuzi wa hoja hiyo, Waziri Mkuu alisema Serikali inawashukuru Waheshimiwa
Wabunge kwa imani kubwa walioionesha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni
huru, juu ya utekelezaji wa majukumu yake, na kuona umuhimu wa kuiongezea
jukumu la kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, Waziri Waziri Mkuu alisema, majukumu ya Tume hiyo,
yameainishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ikiwa ni pamoja na kusimamia Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hivyo, jukumu la kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa
si miongoni mwa majukumu ya Tume kwa mujibu wa Katiba,” alisema.
Katika hatua nyingine, akizungumzia kuhusu uwekezaji kwenye zao la
pamba, Waziri Mkuu alisema
sekta ya pamba na mnyororo wake wote wa thamani ni sekta ya kipaumbele ambayo mbali
na kuwahakikishia soko wakulima na kuongeza kipato chao, uwekezaji katika
viwanda vya nguo unatengeneza ajira nyingi kwa vijana hivyo kuinua kipato chao
na kuboresha maisha ya watu wengi.
“Kwa kutumia mkakati wa kuzalisha nguo na mavazi
mbalimbali (Cotton to Clothing - C2C), Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwa kutumia
teknolojia za kisasa za kutengeneza nguo kuanzia kuchakata pamba hadi nguo kwa
kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafanyika nchini na msisitizo uwe kwenye
utengenezaji wa nyuzi,” alisema.
Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa kwamba bado zao la pamba halijatumiwa vizuri katika kuongeza pato
la Taifa na kuinua maisha ya Watanzania. Pia Wabunge walitaka Serikali ijizatiti
kusimamia uwekezaji kwenye kilimo cha zao la pamba ili kufanikisha utekelezaji
wa mkakati wa viwanda vya nguo nchini wa kufikia malengo ya kuwa Taifa lenye
uchumi wa kati.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi mwaka 2017, ilifanya
tathmini ya kina na kuandaa Blueprint
ambayo imebainisha masuala yote muhimu yanayokwamisha uwekezaji na kuainisha
maeneo yote muhimu yayohitaji kurekebishwa ikiwemo sheria, kanuni na taratibu
zinazosimamia uwekezaji nchini kwa kila taasisi.
Alikuwa akijibu hoja kuhusu umuhimu wa Serikali kufanya tathmini na kuangalia
vikwazo vinavyokwamisha harakati za uwekezaji nchini, kutunga sheria mpya,
kurekebisha baadhi ya sheria ili kuendana na mahitaji ya Blueprint.
Alisema sambamba na hatua hiyo, huduma zimeimarishwa kwa
kuanzisha mifumo ya kielektroniki ambapo wawekezaji wataweza kufanya maombi ya
vibali mbalimbali wakiwa popote bila kulazimika kufika kituoni.
“Mifumo
hii itaondoa urasimu na kuharakisha utoaji wa vyeti vya uwekezaji, leseni na vibali
mbalimbali. Hatua hizi zitapunguza gharama na muda wa mwekezaji kufuatilia
vibali na leseni kwa kila taasisi,” alisema.
Alisema,
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) hivi sasa kina ofisi saba za kanda ambazo ni
Mwanza, Dodoma, Moshi, Kigoma, Mtwara, Mbeya na Dar es Salaam ambazo
zimeanzishwa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wawekezaji.
Bunge
lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/-
kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2019/2020.
Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 62,596,168,581/-
ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile,
Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati
ya hizo sh. 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh.
7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA,
JUMANNE, APRILI 9, 2019.
No comments:
Post a Comment