Na Mwandishi Wetu
MFANYABIASHARA maarufu nchini aliyewahi kuifadhili timu ya
soka ya Simba kwa mafanikio makubwa, Azim Dewji (pichani), ameitabiria makubwa klabu hiyo
katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwishoni mwa wiki hii huko
mjini Lumbumbashi.
Amesema Simba ya mwaka huu ni `moto’ na ina uwezo wa
kuwang’oa Mazembe kutokana na kuundwa na wachezaji wenye vipaji na ari ya
kupata matokeo chanya.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Dewji aliyeifikisha
Simba fainali za Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka 1993, alisema kitu
pekee kinachopaswa kufanywa na wachezaji na viongozi wa Simba ni kuondoa
mchecheto wa mchezo na badala yake kuelekeza nguvu katika mchezo wa marudiano.
“Ni kweli Mazembe ni timu ngumu na kongwe. Ukiangalia ina
historia kubwa Afrika na ndani ya miaka hii kumi tumeshuhudia ikitwaa ubingwa
tofauti wa michuano ya CAF mara tano. Ni rekodi bora sana, lakini
pamoja na ubora wao, nikiangalia ubora na uthubutu wa wachezaji wa Simba, naona
vijana wetu wanaweza kufanya kweli.
“Wachezaji wa sasa wa Simba nawafananisha na wale wa enzi
zile tunafika fainali CAF. Walikuwa wanajituma sana uwanjani. Na hawa
ukiwaangalia wana kila kitu kinachoweza kuwaduwaza Mazembe kwao. Angalia
walivyowakimbiza hapa Dar es Salaam, kwa kawaida Mazembe si wa kujiangusha
hivyo, lakini uliona katika mchezo wa kwanza, walizidiwa sana ila bahati
haikuwa kwa Simba.
“Na hata hao wanaobeza penalti ya John Bocco watambue Simba
hii ni moto wa kuotea mbali na usishangae kuona mpira umetangulia Lubumbushi na
wachezaji wanakwenda kumalizia kazi ya kuandika historia zaidi kwa soka ya
Tanzania,” alisema Dewji.
Kumkataa mwamuzi
Akizungumzia tukio la klabu hiyo kupinga kubadilishiwa
mwamuzi wa mchezo wa marudiano dhidi ya Mazembe, alisema jambo hilo
litawarejesha mchezoni wachezaji, lakini pia kuongeza umakini wa waamuzi katika
mchezo huo.
“Hata kama CAF hawatabadilisha uamuzi huo, mwamuzi
aliyepangwa (Janny Sikazwe wa Zambia) atakuwa makini zaidi na kizuri ni kwamba
hatataka kuharibu sifa zake zilizomwezesha kuchezesha michuano karibu yote
mikubwa duniani. Amechezesha Kombe la Dunia mara mbili, Kombe la Mataifa ya
Afrika mara mbili, pia fainali za Klabu Bingwa ya Dunia, achilia mbali hii
michuano ya klabu Afrika,” alisema Dewji aliyewataka Watanzania kuendelea
kuwaunga mkono wawakilishi hao wa taifa.
Katika mchezo wa kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita jijini
Dar es Salaam, timu hizo hazikufungana, hivyo kuzifanya timu zote kuwa na
nafasi ya kusonga mbele hatua ya nusu fainali, matokeo ya mwishoni mwa wiki
yakiwa mwamuzi wa mwisho.
No comments:
Post a Comment