Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisoma Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020, Bungeni jijini Dodoma jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
UZALISHAJI mdogo wa zao
la Michikichi ni miongoni mwa sababu za kushindwa kujitosheleza kwa mahitaji ya
mafuta ya kula nchini na Serikali imekuwa ikilazimika kutumia fedha nyingi za
kigeni kwa ajili ya kununua mafuta hayo kutoka
nje ya nchi.
Kutokana na changamoto
hiyo, Serikali imeamua kuweka nguvu kubwa kwenye uzalishaji wa mazao ya mbegu
za mafuta ili kuondokana na utegemezi na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni.
Hayo yamesemwa leo
(Alhamisi, Aprili 4, 2019) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha hotuba
ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020.
Waziri Mkuu amesema katika
kutekeleza azma hiyo, Serikali imeanza kuimarisha kilimo cha zao la michikichi
hususan katika mkoa wa Kigoma ili kusaidia upatikanaji wa mbegu bora za
chikichi.
Amesema lengo ni
kuzalisha na kusambaza kwa wakulima miche ipatayo milioni 20 katika kipindi cha
miaka minne (2018/2019 hadi 2021/2022), pia Serikali imeamua kukifanya Chuo cha
Maendeleo ya Wananchi Kihinga, mkoani Kigoma kuwa Kituo cha Utafiti wa Mbegu
Bora za michikichi.
“Maamuzi haya ya
Serikali yameanza kuzaa matunda, hadi kufikia Februari 2019, Kituo cha Kihinga
kimezalisha mbegu 4,747 ambazo zimefanyiwa uoteshwaji wa awali. Katika mwaka
2019/2020, Serikali imepanga kuzalisha miche ya michikichi milioni tano.”
Waziri Mkuu amesema matarajio
ya Serikali ni kuhakikisha kwamba usimamizi mzuri wa mkakati huo wa miaka minne
utalisaidia Taifa kuondokana na uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje,
kutengeneza fursa mbalimbali za ajira na kuwaongezea kipato wakulima wa michikichi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hali
ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2017/2018 na upatikanaji wa
chakula kwa mwaka 2018/2019, imeendelea kuimarika.
Waziri Mkuu amesema
hatua hiyo imetokana na hali nzuri ya mvua katika maeneo mengi ya nchi,
kuongezeka kwa tija na uzalishaji. “Uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia
tani milioni 16.89 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya tani milioni 13.57
na kufanya nchi kuwa na ziada ya chakula ya tani milioni 3.32.”
Amesema uzalishaji wa
mazao makuu ya kimkakati yakiwemo chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku
umeimarika kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ikiwemo kuimarisha
ushirika.
“Kwa mfano, uzalishaji
wa zao la pamba uliongezeka kutoka tani 132,934 mwaka 2017/2018 hadi kufikia
tani 222,039 mwaka 2018/2019 wakati uzalishaji wa zao la Kahawa uliongezeka
kutoka tani 45,245 hadi kufikia tani 65,000.”
Waziri Mkuu amesema Serikali
imeendelea kutoa kipaumbele kwa mazao hayo na mengine kwa kuwa ndiyo mhimili wa
kutoa malighafi za kuendesha viwanda na yana mnyororo mpana wenye fursa ya
kutoa ajira nyingi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma,
ALHAMISI, APRILI 4, 2019.
No comments:
Post a Comment