HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 07, 2019

TUTAENDELEA KUMUENZI MAREHEMU SOKOINE-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali na Watanzania wote wataendelea kumuenzi shujaa wao, Marehemu Edward Moringe Sokoine.

Amesema Marehemu Sokoine wakati wa uhai wake alijitoa kuchapa kazi kwa bidii na amelitumikia Taifa kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Aprili 6, 2019) katika mbio za marathon kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 35 ya kifo cha Sokoine. Mbio hizo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Waziri Mkuu amesema Serikali iliamua kwa makusudi kukiita Chuo Kikuu cha Kilimo jina la Sokoine  ili kumuenzi  shujaa huyo.

Amesema Taifana Watanzania kwa ujumla wataendelea kufuata nyayo za Marehemu Sokoine katika mema mengi aliyolitendea Taifa la Tanzania na siku zote watandelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu.

Waziri Mkuu amesema kufanyika mbio hizo za Marathon ni ushahidi kwamba Marehemu Sokoine bado anakumbukwa na kuheshimiwa  na Watanzania kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika ustawi wa Taifa. 

Alisema katika uhai wake, Marehemu Sokoine alikuwa ni mfano bora wa kiongozi wa juu  wa nchi  aliyedhamiria kwa dhati  kupambana na vitendo vya rushwa, uonevu, ubadhirifu na ufisadi.

“Leo hii tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 35 ya kifo cha Sokoine sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Magufuli inayoendeleza kwa vitendo  utendaji, uandilifu na mtazamo aliokuwa nao marehemu Sokoine.” 

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Marehemu Sokoine, mtoto wa Marehemu, Namelok Sokoine alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuwaenzi kwa vitendo waasisi wa Taifa la Tanzania.

Alisema anafarijika kuona kwamba yale yote aliyoyaamini na kuyasimamia Marehemu Sokoine hivi sasa yanatekelezwa kwa kasi zaidi na ufanisi wa hali ya juu na Serikali inayoongozwa Rais Dkt. Magufuli. 

Amesisitiza kwamba   familia ya Marehemu Sokoine  inaunga mkono kwa dhati  juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na inaamini kwamba Tanzania yenye neema inakuja.

Katika Marathon hiyo, washindi kwa uapnde wa wanaume waliokimbia kilomita 21 ni Joseph Panga, mshindi wa kwanza, na wa pili alikuwa ni Aliphonce Felix Simbu na mshindi wa tatu alikuwa Lazaro Damasi.

Upande wa wanawake kilomita 21, mshindi wa kwanza alikuwa ni Faulina Abdi Matanga, mshindi wa pili alikuwa ni Magdalena Shauri na mshindi wa tatu alikuwa ni Nathalia Elisante.

Waliohudhuria katika mashindano hayo ni pamoja na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Wabunge na viongizi pamoja na wengine wa Serikali.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, APRILI 6, 2019.

No comments:

Post a Comment

Pages