WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka taasisi
zinazofanya uhakiki na upimaji bidhaa nchini zijirekebishe na ziongeze kasi ya
utoaji matokeo kwa wateja.
"Kumekuwa na malalamiko kutoka mipakani juu ya
bidhaa zinazochukuliwa ili zikapimwe kwamba zinachukua muda mrefu. Punguzeni
urasmi huo ili kufanya sekta ya biashara iweze kwenda kwa haraka zaidi. Tume yako
(TAEC), TBS na TFDA ni miongoni mwa taasisi zinazolalamikiwa na wawekezaji na
wafanyabiashara. Tumieni fursa hii kujirekebisha na kuharakisha utoaji wa
matokeo," amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Aprili
29, 2019) wakati akizindua maabara ya Maabara ya kisasa ya Teknolojia ya
Nyuklia ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission
-TAEC) iliyopo Njiro, jijini Arusha.
“Nafahamu kuwa hii Tume inafanya kazi kwa karibu na
bandari vituo vya mipakani ili kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini.
Naamini kuanzia sasa mtaharakisha upimaji wa bidhaa na vifaa na kutoa majibu ya
vipimo haraka,” amesema.
Waziri Mkuu ameitaka Bodi na Menejimenti ya Tume,
waendelee kubuni na kuibua miradi mingine zaidi ya matumizi salama ya
teknolojia ya nyuklia. “Angalieni uwezekano wa kuanzisha kinu cha utafiti
kinachotumia teknolojia ya nyuklia (Research Reactor); mtambo wa kuongeza
thamani na ubora wa vitu mbalimbali ikiwemo matunda na mazao mbalimbali
(multi-purpose irradiator); na mtambo wa kuzalisha dawa za kuchunguza na kutibu
maradhi ya saratani (accelerator).”
Amesema kwa kufanya hivyo, maabara hiyo na watumishi
wake wataongeza mchango wa teknolojia ya nyuklia kwenye ustawi wa jamii na
ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema anatambua kwamba Tume ya Nyuklia Tanzania
inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa wafanyakazi na ufinyu wa
bajeti ya ujenzi wa maabara awamu ya pili. “Serikali inazichukua changamoto
hizo na itaendelea na juhudi za kuzitafutia ufumbuzi kadiri hali ya kiuchumi
itakavyoruhusu,” amesema.
Waziri Mkuu ameishukuru Jumuiya ya Ulaya kwa msaada
wa vifaa vya maabara hiyo vyenye thamani ya Euro milioni 2.2 (sawa na sh.
bilioni 7.5) na kwamba Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika sekta
mbalimbali.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu ameiagiza Bodi na uongozi wa Tume hiyo wawapandishe vyeo
watumishi watatu wa tume hiyo ambao aliwapa vyeti na zawadi ya sh. milioni moja
kila mmoja kwa kukataa rushwa na kutokubali vitisho walivyopewa.
“Nimefurahi sana kuona watumishi watatu ambao ni
wazalendo na wamekataa kupokea rushwa au kukubali vitisho walivyokuwa wakipewa
na kuamua kusimamia misingi ya kazi zao. Hii zawadi mliyowapa haitoshi.”
“Watumishi hawa ni mfano wa kuigwa na wengine.
Mwenyekiti wa Bodi waongeze fedha nyingine kila mmoja sh. milioni mbili ili
jumla iwe milioni tatu na wapandishwe vyeo huko waliko ili iwe motisha zaidi
kwao. Sijui muundo wenu ukoje, lakini nataka nipate taarifa ya utekelezaji wa
haya maamuzi kesho kutwa, baada ya Mei mosi,” amesisitiza.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu awape vyeti na zawadi, Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Najat
Mohamed aliwataja watumishi hao kuwa ni Machibya Matulanya wa kituo cha Mtwara
na mpaka wa Kilambo (Tanzania) na Msumbiji; Patrick Simpokolwe na Geofrey
Kalolo wa kituo cha Tunduma (Tanzania) na Zambia.
Machibya Matulanya ambaye cheo chake ni mtafiti wa
mionzi daraja la pili (Radiation Health Physics Research Officer II) amekuwa
akitegewa mitego ya rushwa na kupokea vitisho kutoka wa wafanyabiashara na
watumishi wa Serikali.
Patrick Simpokolwe ambaye cheo chake ni mkaguzi wa
usalama wa mionzi daraja la pili (Radiation Safety Inspector II) na Geofrey
Kalolo ambaye ni mtumishi wa kujitolea (volunteer) naye pia anafanya kazi kama
mkaguzi wa usalama wa mionzi daraja la pili. Wote kwa pamoja walipokea vitisho
walipozuia mzigo kutoka Zambia wenye thamani ya zaidi ya milioni 20 usiingizwe
nchini.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
APRILI 29, 2019.
No comments:
Post a Comment