Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mhe.
Stephen Wasira akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati alipowasili katika Chuo hicho
kufungua Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameutaka uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu
ya Mwalimu Nyerere kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuona namna bora ya kuhuwisha mitaala ya Chuo hicho ili kifikie viwango vya
Elimu ya Juu.
Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo
Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya Kumbukizi ya
Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo amesema mpaka sasa Chuo hicho kimekidhi viwango vya
kuwa na hadhi ya Chuo Kikuu na kwamba elimu inayotolewa katika chuo hicho ndio
inasisitizwa nchini.
Ameutaka uongozi wa chuo hicho
kutia mkazo katika mafunzo ya uongozi na maadili hususan yale yenye mwelekeo wa
kujenga uzalendo na kuendelea kutumia fursa ya uwepo wa makongamano kukuza
uelewa wa jamii ya watanzania kuhusu umuhimu wa kuenzi falsafa za mwalimu katika
umoja, upendo, uzalendo, uadilifu na mshikamano wa kitaifa.
Aidha Mhe. Majaliwa amesema
Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa kujenga misingi ya Amani, umoja na
kuleta maendeleo ya jamii nchini kwa vitendo na kuwataka watanzania kuzingatia
maadili, uzalendo na utaifa katika uwajibikaji
wa kila siku, kuungana kwa pamoja bila kujali itikadi za kisiasa au
kabila katika kulinda na kudumisha tunu hizo.
“Nimpongeze Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi anazochukua ili
kuhakikisha anairejesha nchi yetu kwenye misingi yake ya awali ambayo ni kuwa
na viongozi waadilifu, wazalendo na wenye kulinda Amani na kudumisha umoja
katika jamii, watanzania wote tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi na kuzilinda
kwa nguvu zote,” alisema Mhe. Majaliwa.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako
amesema ni vizuri kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere kwa kuwa ni mtu ambaye amelipigania Taifa na kuliletea ukombozi na
kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufuata nyayo za Baba wa Taifa.
Waziri Ndalichako ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa
wanafunzi katika kongamano hilo kwa kuwa linawapa fursa ya kupata uelewa mpana
wa zaidi ya kile wanachofundishwa shuleni, na kwamba taifa linawategema kuwa
chachu ya mabadiliko katika nchi.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya uendeshaji wa Chuo cha Kumbu Kumbu
ya Mwalimu Nyerere Steven Wassira alimweleza Waziri Mkuu kuwa wanaomba katika
kumenzi Baba wa Taifa Chuo hicho kipandishwe hadhi na kuwa Chuo Kikuu na kwamba
mazingira yake yaboreshwe yawe na hadhi ya Hayati Baba wa Taifa.
Kwa upande wake mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere,
Prof. Shadrack Mwakalila amesema, uongozi wa chuo hicho unaendelea na maboresho
ya kutoa taaluma yenye kujenga uzalendo kwa vijana wa kitanzania.
Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa
limechagizwa na mada isemayo Mchango wa Mwalimu Nyerere katika kujenga Amani,
umoja na Kuleta Maendeleo ya Jamii nchini.
Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
11/04/2019
No comments:
Post a Comment