HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 02, 2019

YANGA KUPATA VIONGOZI WAKE MEI 5

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Malangwe Mchungahela, akionyesha leja ya wanachama wa Yanga  wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelekea uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika Mei 5. (Picha na Mtandao).


Dar es Salaamm, Tanzania


FAINALI ya michuano ya Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (2019 AFCON U-17), itakayopigwa Aprili 28 jijini Dar es Salaam, imelilazimu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusogeza mbele hadi Mei 5 Uchaguzi Mkuu wa viongozi wa klabu ya Yanga.


Machi 26 mwaka huu wajumbe wawili waliokuwa wamesalia katika nafasi za uongozi ndani ya Yanga, Samuel Lukumay na Hussein Nyika, walitangaza kujiuzulu nafasi zao kupisha Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo, ambao ulitangazwa kufanyika Aprili 28.

Tarehe hiyo ya uchaguzi ilitangazwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, George Mkuchika, ambaye aliwataja wajumbe saba wa kuiongoza Yanga kuelekea uchaguzi uliokuwa ufanyike mwakani, ila ukarudishwa mwaka huu ili kupisha uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge.

Kamati ya muda ya kuiongoza Yanga iliyotangazwa na Mkuchika inaongozwa na Lucas Mashauri (M/kiti), Said Ntimizi (Makamu), wajumbe ni Hussein Ndama, Moses Katabaro, Maulid Kitenge, Nyika pamoja na Lukumay, jukumu kuu likiwa ni kuhakikisha Yanga inaenda kabla ya kupata viongozi.

Mkuchika akaenda mbali kwa kutangaza Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, chini ya Mwenyekiti Mwanasheria Sam Mapande, wajumbe wakiwa ni Daniel Mlelwa, Mustafa Nagali, Godfrey Mapunda, Edward Mwakingwe, Issa Nguvu, Venance Mwamoto, Seif Gulamali na Dastan Kitandula.

Siku mbili baada ya Mkuchika kutangaza Uchaguzi Mkuu wa Yanga kufanyika Aprili 28, Serikali ililitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kushirikiana na TFF ili kuhakikisha Yanga inafanya uchaguzi na kupata viongozi wake ndani ya siku 30.

Licha ya Serikali kutaka Yanga iwe imekamilisha mchakato huo ndani ya siku 30, TFF haikuweza kurudisha nyuma siku hiyo, kwani itakuwa ‘bize’ na fainali za vijana, ambazo Tanzania itacheza kama mwenyeji kupitia kikosi cha Serengeti Boys, hivyo kulazimika kusogeza kwa wiki moja.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela, alisema Aprili 28 waliyochagua Yanga, inaingiliana na fainali za vijana AFCON U-17), itakayofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchungahela alisema kuwa, wameitikia mwito wa awali wa wanachama wa Yanga kutaka jukumu la kufanikisha uchaguzi liachwe mikononi mwao na kusema kila kitu kitafanywa na Yanga wenyewe na wao kama TFF watabaki kuwa wasimamizi pekee. 

"Uchaguzi wa Yanga utakuwa Mei 5 na kila kitu kitafanywa na Yanga wenyewe sisi TFF tutakuwa waangalizi," alisema Mchungahela, huku akisema kwa wagombea wa uchaguzi wa awali ulioota mbawa, watabaki katika nafasi zao, au kama wataomba vinginevyo.

Mchungahela alitoa ratiba ya uchaguzi huo kuwa mchakato wa kuchukua fomu unaanza rasmi leo Aprili 2 na utafungwa Aprili 7.

Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, kitakachofuata Kikao cha mchujo kwa wagombea, kitakachofanyika Aprili 9, kabla ya Aprili 10 kubandikwa kwa majina yatayopitishwa kuwania nafasi mbalimbali. Siku tatu za pingamizi zitaanza Aprili 11 hadi 14, kabla ya kuzipitia pingamizi na usaili Aprili 16 hadi 18.

Kwa mujibu wa ratiba ya Mchungahela, Aprili 18 hadi 23 itakuwa siku tano za Sekretariati kusikiliza maamuzi ya Kamati ya Maadili, kabla ya Aprili 24 hadi 26 kutumika kukata rufaa.

Rufaa zitakazokatwa zitasikilizwa kwa siku tatu, yaani Aprili 27 hadi 29, kabla ya kampeni kuanza kuchukua nafasi Aprili 30 hadi Mei 4, kisha uchaguzi mkuu kufanyika Mei 5 mwaka huu, kupata viongozi watakaodumu madarakani kwa miaka minne kama katiba ya Yanga inavyosema.

Wakati hayo yakijiri, jumla ya wachezaji 20 wa kikosi cha Wana Jangwani hao, leo alfajiri kinaanza safari kueleka Mtwara tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), dhidi ya wenyeji Ndanda FC.

Ndanda FC watawaalika Yanga katika mfululizo wa TPL, mchezo uliopangwa kutimua vumbi, Alhamisi hii Aprili 4 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, Yanga itaendelea kukosa huduma za nahodha wake Ibrahim Ajib, ambaye atakosekana kikosini kutokana na majeraha madogo aliyonayo, lakini itakuwa na marejeo ya beki wa kulia (asiye na namba kikosini), Juma Abdul.

"Ibrahim Ajib bado tutaendelea kumkosa kikosini kutokana na majeraha ya mguu, lakini jambo jema ni kwamba Juma Abdul amerejea kikosini na atakuwa sehemu ya msafara wa kikosi chetu. Tunaamini mchezo utakuwa mgumu, lakini maandalizi tuliyoyafanya yanatosha kutupa matokeo mazuri," alisema Ten.

No comments:

Post a Comment

Pages