Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dk. Philip Mpango (kushoto), akipeana mkono na mgeni wake Rais wa
Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Bw. Gilbert Fossoun Houngbo, katika
Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Na
Peter Haule, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Mfuko
wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Gilbert Houngbo, na kuiomba
Taasisi hiyo kusaidia kuendeleza zaidi Sekta ya Kilimo kupitia mpango wake mpya
wa awamu ya 11 wa kuendeleza kilimo
nchini.
Dkt. Mpango ameyataja baadhi ya maeneo ya
kipaumbele kuwa ni uzalishaji wa mbegu bora, kusaidia kilimo cha umwagiliaji,
kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima, kusaidia upatikanaji wa mitaji
kwa wakulima na kuanzisha taasisi za utafiti wa kilimo za kikanda.
Aidha, Dkt. Mpango alimwomba kiongozi huyo kusaidia
pia mbinu za kupunguza upotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno ili kuchochea
na kuongeza tija katika sekta ya kilimo ambayo amesema inaajiri zaidi ya
asilimia 66 ya Watanzania.
”Takiribani asilimia 66 ya watanzania wanategemea
kilimo na kilimo ndio mwajiri mkuu hivyo kwa kuwa IFAD ina program mpya,
tumeamua kushauriana ili wajue vipaumbele vya Serikali na fedha tutakazo zipata
tuzielekeze katika maeneo hayo”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema kuwa
Serikali inaunda kikosi kazi kitakacho husisha Wizara ya Kilimo, Wizara ya
Fedha na Mipango na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili kuweka nguvu ya pamoja kwa
kuangalia maeneo ya vipaumbele ambavyo Mfuko wa IFAD utasaidia.
Kwa upande wake Rais wa IFAD Bw. Gilbert Houngbo,
alisema kuwa Taasisi yake itashirikiana na Tanzania katika jitihada zake za
kupunguza umasikini wa wananchi kupitia kilimo kwa kuyapatia ufumbuzi masuala
kadhaa ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa mbolea na mbegu bora za kilimo na
mifugo, masoko ya bidhaa, upatikanaji wa mitaji, kuongeza ujuzi wa wakulima,
kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na kuwashawishi vijana wengi kujihusisha na
kilimo.
Alielezea kufurahishwa kwake na mwamko pamoja
na mwitikio wa baadhi ya wakulima na wafugaji walionufaika na awamu
zilizotangulia za uendelezaji sekta ya kilimo na mifugo kupitia taasisi yake aliowatembelea,
ambao amesema wanamtazamo mzuri wa
kilimo cha kibiashara kinachozingatia uongezaji wa mnyororo wa thamani, suala
ambalo ni moja ya lengo la Mfuko huo katika kuendeleza Sekta hiyo.
Mfuko
wa IFAD ulianza
kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya maendeleo ya kilimo kuanzia
mwaka 1978,
ambapo hadi sasa imesaidia miradi 15 yenye thamani ya dola za Marekani
milioni 385.80 na katika awamu mpya ya miaka mitatu kuanzia mwaka
2019/2021, IFAD imetenga zaidi ya dola za Marekani milioni 58.8 kwa
ajili ya kuendeleza Sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na kuwasaidia wakulima kutumia
teknolojia ya kisasa ya kilimo na mifumo ya masoko, kuhamasisha Sekta binafsi
katika uwekezaji na kuwasaidia wakulima wadogo na wavuvi kuongeza kipato na
kupunguza umasikini kwa kuzingatiakuongeza mnyororo wa thamani ya mazao husika.
Sekta ya Kilimo nchini
inachangia asilimia 30.1 ya jumla ya pato la ndani (GDP), asilimia 26 ya mapato
ya kigeni, ajira takribani asilimia 65.5, inachangia malighafi za viwandani kwa
takribani asilimia 65 na inachangia
kwenye mahitaji ya chakula kwa asilimia 100.
No comments:
Post a Comment