Na
Mwandishi Wetu
Wizara
ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu
imewataka wapenzi na wadau wa soka nchini kushiriki maandalizi ya mashindano ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki (CECAAF) yanayotarajiwa
kufanyika nchini Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Mei 16, 2019 Jijini Dodoma,katika mkutano
uliolenga kuitambulisha kamati ya wabunge watano waliojitolea kuhamasisha
Watanzania,kushiriki kwa hali na mali katika mashindano hayo, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
Dkt. Harrison Mwakyembe, amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha nchi za
Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya na Rwanda.
“Mashindano
haya yatakayokuwa ya kwanza kufanyika katika ukanda huu wa Afrika yameanzishwa
kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za Walemavu wa mwaka 2006,
unaotaka haki ya Walemavu kushiriki katika mambo kadhaa ikiwemo michezo”
Akifafanua
zaidi, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa lengo la kuhamasisha umma wa watanzania ni
kuunga mkono mashindano hayo kwa hali na mali.
Kwa
upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri
mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu Mhe. Stella Ikupa amesema kuwa mashindano
hayo yatasaidia kuibua vipaji vya watu wenye ulemavu na hivyo kushiriki katika
kukuza sekta ya michezo.
Pia
ameiomba jamii kwa upana kujitokeza kuchangia na kushiriki mashindano hayo kwa
kuzingatia kuwa watu wenye ulemavu wana nia ya kushiriki vyema katika
mashindano hayo.
Naye
mbunge wa Sengerema mhe. William Ngeleja,ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya
michezo ya Bunge, akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, amesema kuwa watashiriki kikamilifu katika
kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanikiwa kwa kuzingatia malengo yake.
Mheshimiwa
Ngeleja,aliongeza kusema kuwa watashiriki kwa vitendo kwa kuzingatia kuwa Bunge ni wasimamizi wa sheria
za sekta ya michezo ,mikataba ya kimataifa, sheria na kanuni katika sekta hii.
Wizara
ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, inawaomba wananchi kuipa
Kamati hii ya wabunge ushirikiano wakutosha katika maandalizi ya michuano hiyo
ambayo inahitaji fedha ya kutosha na vifaa.
Wabunge
wanaounda kamati hiyo ni Mheshimiwa William Ngeleja,Mheshimiwa Venance
Mwamoto,Mheshimiwa Margareth Sitta, Mheshimiwa Amina Mollel na Mheshimiwa Riziki
Said Lulida.
No comments:
Post a Comment