HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 28, 2019

Dk.Tairo:Utafiti wa GMO unaendelea

 Mratibu wa Utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk.Fred Tairo akitoa mada kwenye mjadawa kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO).

Na Suleiman Msuya

SERIKALI imesema utafiti kuhusu Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO), unaendelea katika vituo vya Utafiti Kilimo Mikocheni (MARI) na Shamba la Majaribio
 Makutupora Dodoma.

Kauli ya Serikali kuendelea na utafiti wa GMO inakuja ikiwa ni takribani miezi minne imepita baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigimwa kutangaza uamuzi wa Serikaki kusitisha utafiti huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mratibu wa Tafiti za Bioteknolojia za Kilimo nchini Dk. Fred Tairo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Mikocheni (TARI Mikocheni), wakati akiwasilisha mada ya hali ya utafiti wa GMO nchini kwenye mkutano wa mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO ulioandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala  ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema wao wanaendelea na utafiti katika vituo husika.

Dkt. Tairo alisema TARI haijaacha kufanya utafiti wa GMO tangu walivyoanza na kwamba utafiti umeonesha matokeo chanya.

Alisema taarifa zilizokuwa zimesambazwa kuwa utafiti huo umesitishwa hazikuwa sahihi na kwamba wanaendelea na utafiti katika hatua mbalimbali.

"Baadhi ya vyombo vya habari na wananchi walielewa vibaya kauli iliyotolewa serikali ilitaka watafiti wafuate utaratibu wa kutoa matokeo waliyokuwa wanayapata kwenye majaribio hayo ili kuondoa mkanganyiko," alisema Tairo.

Mtafiti huyo alisema utafiti wa GMO TARI Mikocheni na Makutupora unaendelea na utakapokamilika matokeo yake yatawasilishwa serikalini kwaajili ya kufanyiwa maamuzi ya kuitumia au kutoitumia.

Mratibu huyo wa Bioteknolojia alisema umuhimu wa serikali kufanya tafiti za GMO ni kukabiliana na changamoto sugu zinazotokana na madiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame, wadudu na magonjwa sugu ili kuongeza tija kwa wakulima.

Alisema kuwa majaribio yanayofanyika katika taasisi ya utafiti ya Makutupora mkoani Dodoma unalenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya ukame na bungua wa mahindi na kwa matokeo ya awali yameonyesha kufanikiwa pia kupambana pia na Viwavi jeshi vamizi.

Dk. Tairo alisema TARI imefanya utafiti kwa upande wa zao la Muhogo ambao unalenga kuipa kinga mihogo kupambana na magonjwa sugu ya batobato kali na michirizi ya kahawai ambayo yanaathiri sana zao wakulima wa muhigo afrika hasa kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mtafiti huyo alisema GMO imeonesha kuwepo na matokeo chanya ya chakula, rutuba, usalama wa chakula na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Napenda kuweka wazi Tanzania ipo katika hatua ya pili ya utafiti ambao ni wa kwenye shamba maalum baada ya kumaliza ule wa ndani unaofanyika MARI. Nasisitiza kuwa hakuna bidhaa ya GMO inaayozalishwa nchini," alisema.

Kwa upande wake Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, Mashamba Philipo, alisema teknolojia hiyo ni nzuri ila serikali, wakulima na watafiti wanapaswa kukaa pamoja kuona kama ni muda muafaka wa teknolojia hiyo kutumika hapa nchini.

Mtafiti huyo alisema teknolojia hiyo ina uwezo wa kuwezesha nyanya kuwekewa Jeni ambayo inauwezo wa kuifanya isiharibike ndani ya mwezi mmoja hata baada ya kuichuma na hivyo kumuongezea tija mkulima.

Philipo alisema teknolojia hiyo sio ngeni duniani kwa kuwa inatumika nchi mbalimbali kama Marekani, China, Brazil na nyingine nyingi za afrika zinaitumia lakini ni muhimu wadau wote wapewe elimu ili kuondoa mashaka waliyoona kuhusu teknolojia hiyo.

Mtafiti Emmanuel Sulle ambaye ni Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Western Cape Afrika Kusini alissema kuna haja ya serikali kuongeza bajeti kwenye tafiti za kilimo nchini ili kuwezesha watafiti  kupatafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima.

Sulle alisema pia Serikali inawajibu wa kuongeza idadi ya watafiti kwenye utafiti wa aina hiyo ambao unakuwa kwa kasi duniani ili waweze kuwa na uwezo wa kufanya tafiti hizo katika viwango vinavyotakiwa kimataifa.

Alisema pamoja na kufanya tafiti za GMO lakini lazima watafiti waangalie mbinu zingine za asili wanazozitumia wakulima na kuziboresha na kuongeza uzalishaji.

No comments:

Post a Comment

Pages