HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 06, 2019

ESPERANCE KUISHTAKI CAF, WAGOMA KURUDIA FAINALI MABINGWA AFRIKA

 Esperance waakishangilia taji.
 Nahodha wa Wydad Casablanca, Abdelatif Noussir, akimlalamikia mwamuzi kutoka  Gambia, Bakary Gassama.
 Wachezaji wa Wydad wakiombwa kurudi uwanjani kuendelea na mchezo wa fainali.

Tunis, Tunisia

BAADA ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwapa saa 72 klabu ya Esperance ya Tunisia kurejesha Kombe na medali za Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) na kutangaza kufuta matokeo yote ya mechi mbili za fainali dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, Esperance imegomea maamuzi.

Fainali ya pili ya CAF Chaampions League, ilivunjika dakika ya 61 kwenye dimba la Rades Olympique mjini Rades, Tunisia, baada ya Wydad kugomea uamuzi wa kulikataa bao lao la kusawazisha na walipotaka kutazamwa kwa video za uamuzi (VAR), ilibainika hazifanyi kazi, hivyo kukataa kuendelea na mchezo. 

Katika fainali hiyo ya marudiano, Wydad walikuwa wakihitaji ushindi ama sare inayoanzia mabao 2-2 ili kuwavua taji Esperance, baada ya mechi ya kwanza kwenye dimba la Prince Moulay Abdellah, kumalizika kwa sare ya bao 1-1, lakini mwamuzi Bakary Gassama, alilikataa bao la kuchomoa la Wamorocco hao na kususia mechi.

Licha ya jitihada za viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa CAF, Ahamad Ahamad, Wydad walishikilia msimamo wa kutocheza, ambako Gassama alisubiria kwa dakika kadhaa kisha kuvunja pambano na kuwapa ushindi Esperance waliokuwa wakitetea taji lao. 

Ni uamuzi uliopata ukosoaji mkubwa duniani, huku wadau wakihoji uhalali wa kuendesha fainali moja kwa teknolojia ya VAR, kisha marudiano hayo kukwama kufanya hivyo. Ndipo Kamati Tendaji CAF ilipokutana juzi na kuagiza Esperance warejeshe Kombe na medali za ubingwa, kupisha mechi ya kurudia.

Katika maamuzi hayo, CAF ilisema pambano hilo litapigwa katika uwanja huru huko nchini Afrika Kusini baada ya fainali za Mataifa Afrika, na kwamba utachezeshwa na waamuzi kutoka Ulaya.

Sasa wakati Wydad Casablanca wakifurahia maamuzi hayo kutoka CAF, Esperance haijakubaliana nayo kwa kusema wao hawajasababisha mechi hiyo kuvunjika na wamesema wataenda kuishitaki CAF kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS) kuhusu uamuzi wao wa kutaka kurudia mechi ya fainali.

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Tunisia (FTF), Wesif Jalil, ameyaita maamuzi ya CAF ya kutaka marudio ya fainali hiyo kuwa ni yasiyo ya haki na kuongeza: "Tumeshtushwa na maamuzi haya na kimsingi tunayaona yasio ya haki na tunasema wazi tutayapinga kwa sababu hayajazingatia shreria." 

Jalil aliongeza kuwa kosa lilifanywa na Wydad na sio Esperance sasa wanashangaa kuona maamuzi ya aina hiyo, ambayo hayajui yametokana na sheria ama kanuni ipi na kusisitiza: "Kila mmoja anajua kwanini mechi ilisimama na nani aligomea mechi? Bila shaka ni Wydad, sasa inakuwaje irudiwe.?

No comments:

Post a Comment

Pages