Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe akizungumza na
Watumishi wa ofisi hiyo (hawapo pichani) alipokutana nao kujadili utendaji kazi
ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe amewaasa watumishi
wa ofisi hiyo kufanyakazi kwa ushirikiano ili waweze kutumiza malengo waliyojiwekea.
Hayo ameyasema wakati
alipokutana na watumishi wa ofisi yake Dodoma kwa lengo la kuadhimisha Wiki ya
Utumishi wa Umma inayofanyika kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi 23 kwa Nchi Wanachama
wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kuonesha mchango wa Watumishi wa Umma
katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla ambapo kauli mbiu ya
mwaka huu ni;
“Uhusiano kati ya uwekezaji
wa vijana na usimamizi wa masuala ya uhamiaji: Jenga utamaduni wa Utawala bora,
matumizi ya TEHAMA na Ubunifu katika utoaji wa huduma jumuishi.”
Katika kuadhimisha Wiki ya
Utumishi wa Umma ambayo ipo kisheria Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Ofisi hiyo
ina majukumu makubwa ya kiutendaji hivyo watumishi wanawajibu wa kufanyakazi
kwa kushirikiana na kujenga umoja.
“Ushirikiano katika kazi ni
muhimu na husaidia kuboresha mifumo ya kiutendaji ikiwemo kuwa na mikakati
endelevu ya ofisi, mawasiliano mazuri, kujenga mahusiano mazuri na wadau na
kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Massawe.
Sambamba na hilo aliwasihi
watumishi wa ofisi hiyo kufanyakazi kwa bidii, weledi, uzalendo na kuwa wabunifu
katika kutekeleza majukumu yao na utoaji wa huduma kwa wadau na wananchi.
Pia amewashauri watumishi
hao kuepukana na vitendo vya rushwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na maadili ya
Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia haki na
usawa.
Aidha, Katibu Mkuu alikutana
na kufanya kikao na wadau mbalimbali wa nje na alipokea maoni na mrejesho wa
huduma zinazotolewa na Ofisi ya Waziri kuhusu sekta ya Kazi, Maendeleo ya
Vijana, Ajira, Huduma kwa Watu wenye Ulemavu, Hifadhi ya Jamii na masuala ya
Vyama vya Wafanyakazi.
Naye Mkurugenzi wa Utawala
na Rasilimali Watu Bw. Peter Kalonga aliafiki yaliyosemwa na kuahidi kuahidi
kufanyia kazi maagizo hayo ikiwemo suala la ushirikiano na mawasiliano katika
utendaji kazi baina ya watumishi ili kuimarisha mshikamano baina ya watumishi.
Kwa upande wake alisema kuwa
kikao hiko kimewezesha watumishi wa ofisi hiyo kubadilishana taarifa zaidi za
kiutendaji na kitasaidia kuimarisha ushirikiano baina yao.
No comments:
Post a Comment