HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 22, 2019

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KWA KUFANYA USAFI WA MAZINGIRA


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa ofisi yake mara baada ya watumishi hao kukamilisha zoezi la usafi wa mazingira eneo la Mtumba jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2019. (Picha na Happiness Shayo).

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Fabian Pokela akimwagilia maji moja ya mti uliopandwa katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora eneo la Mtumba jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2019.

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya usafi katika ofisi yao iliyopo Mji wa Serikali, eneo la Mtumba jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2019.
 
 
Dodoma Tanzania
 
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wameadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya usafi wa mazingira katika ofisi yao iliyopo Mji wa Serikali, eneo la Mtumba, jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewapongeza watumishi wa ofisi yake kwa kuadhimisha Wiki hiyo kwa kufanya usafi wa mazingira na kumwagilia maji miti iliyopandwa kuizunguka ofisi.

 “Ni jambo zuri sana kufanya usafi wa mazingira katika siku kama ya leo kwani mmetoa taswira nzuri kwa watumishi wengine na umma kwa ujumla”. Dkt. Ndumbaro amesema.
Aidha, Dkt. Ndumbaro ametoa wito kwa watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu mkubwa ili kuujenga utumishi wa umma kuwa uliotukuka katika Tanzania mpya ambayo Mhe. Rais amedhamiria kuijenga.

Sanjari na hilo, Dkt. Ndumbaro amewataka watumishi hao kuwahudumia vizuri watumishi wa umma na wadau wengine wanaokuja kupata huduma, ikizingatiwa kuwa wanatoka katika maeneo mbalimbali ya nchi yakiwemo ya pembezoni.

“Muelewe kuwa, watumishi na wadau wanaokuja kupata huduma wametoka mbali na wanatumia gharama kubwa na wengine wanakuwa na msongo wa mawazo, hivyo wahudumieni inavyostahili” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni ya mwaka husika. Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka huu imeadhimisha wiki hii kwa kutoa huduma mahala pa kazi, kusikiliza kero na malalamiko ya wateja pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika ofisi yake iliyopo katika Mji wa Serikali, eneo la Mtumba jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Pages