Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Uuzaji Nyumba 4000 katika eneo la
Vingunguti Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya PMM 2001 Ltd inayonunua nyumba
hizo walipokutana katika ofisi za Wizara jijini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati
wa kutafuta muafaka wa ununuzi nyumba hizo. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo
la Segerea Bona Kamoli, wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kamati Ramadhani Pepo,
wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utumishi wa Kampuni ya PMM 2001 Ltd
Damian Kanuti na wa tatu kushoto ni Katibu wa Kamati Ibrahim Mkumbi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akimsikiliza Katibu wa Kamati ya Kusimamia Uuzaji Nyumba 4000 katika eneo la
Vingunguti Dar es Salaam Ramadhani Pepo alipokutana na Kampuni ya PMM 2001 Ltd
inayonunua nyumba hizo pamoja na Kamati jijini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati
wa kutafuta muafaka wa ununuzi nyumba hizo. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo
la Segerea Bona Kamoli, wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utumishi wa
Kampuni ya PMM 2001 Ltd Damian Kanuti na wa tatu kushoto ni Katibu wa Kamati
Ibrahim Mkumbi.
Na Munir Shemweta, DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza kupitiwa upya
Mkataba wa Mauziano ya nyumba baina ya Kampuni ya PMM 2001 Ltd na Wamiliki wa
nyumba 4000 wakazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo unafuatiwa
kutozingatiwa kwa masharti ya Mkataba ulioingiwa awali ambao umeonekana kuwa na
mapungufu mengi ya kisheria na hivyo kusababisha kampuni ya PMM 2001 Ltd
kushindwa kuwalipa Wamiliki wa nyumba katika eneo la Vingunguti kwa takriban
miezi tisa kama walivyokubaliana jambo lililozua taharuki kwa wamiliki wa
nyumba hizo.
Dkt Mabula alitoa agizo
hilo mwishoni mwa wiki baada ya kukutana na pande zote mbili za Kamati
inayosimamia makubaliano ya uuzaji nyumba 4000 katika mitaa minne ya Vingunguti
ambayo ni Mnyamani, Mtambani, Mtakuja na Faru, kampuni ya PMM 2001 Ltd na
Mbunge wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, baada ya kupitia Mkataba wa mauziano ya
nyumba katika eneo la Vingunguti kati ya Kampuni ya PMM 2001 Ltd na Wamiliki wa
nyumba katika eneo la Vingunguti wamebaini mkataba kutofuata taratibu za kisheria
na kubainisha kuwa wamiliki ambao hawajalipwa fedha yoyote hawabanwi na mkataba
huo na wanaweza kuzifanyia shughuli yoyote nyumba zao.
Alisema, kwa zile
nyumba themanini (80) ambazo kampuni ya PMM 2001 Ltd ilizinunua kwa wamiliki
katika eneo hilo, Wizara yake itatuma timu maalum kufuatilia iwapo Kampuni hiyo
imefuata taratibu zote za mauziano ikiwemo kutoa kodi ya serikali na kuongeza
kwa kuitaka kuhakikisha inakamilisha taratibu
za kumilikishwa nyumba hizo..
Akigeukia suala la Wamiliki
wa nyumba 17 ambao kampuni hiyo imewalipa shilingi milioni 35 kwa kila mmoja
kama fedha za awali, Naibu Waziri wa Ardhi aliagiza hatua za kisheria zifuate
kwa kuwa Mkataba wa Mauziano hauoneshi kiasi kilichobaki baada ya kutolewa cha awali
sambamba na muda wa ukamilishaji malipo jambo lililosababisha Wamiliki kufuatilia
kwa muda mrefu bila mafanikio.
Kwa mujibu wa Dkt
Mabula, ilichofanya kampuni ya PMM 2001 Ltd kwa Wamiliki ni udanganyifu
unaoweza kutoa mwanya mkubwa kupoteza
haki yao na kusisitiza kuwa Serikali ya awamu ya tano haiko tayari kuona wananchi
wanapata tabu kufuatilia haki zao na kuiagiza kampuni hiyo kuwaeleza
Wamiliki itawalipa lini kiasi kilichobaki ili kuondoa mkanganyiko.
Hata hivyo, Dkt Mabula
alisema, atamuagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam
kuzungumza na wananchi wanaouza nyumba kwa kampuni hiyo na yeye mwenyewe atakupokuwa
mkoani humo katika ziara yake atazungumza na wakazi hao wa Vingunguti kuhusiana
na sakata hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Fedha na Utumishi wa Kapmuni ya PMM 2001 LTD Damian Kanuti alijitetea kwa
kueleza kuwa kampuni yake ilishindwa kutekeleza makubaliano ya ununuzi wa
nyumba katika mitaa ya Vingunguti kutokana na kuchelewa kupata mkopo ilioutarajiwa
kutoka Benki ya TIB na kubainisha kuwa pamoja na sakata hilo lakini kampuni yake
ilishalipa kiasi cha bilioni 1.7 ikiwa ni malipo ya nyumba 80 na fedha ya awali
kwa Wamiliki 17.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kusimamia Uuzaji nyumba 4000 katika eneo la Vingunguti Ramadhani Pepo
ameilalamikia kapuni ya PMM 2001 Ltd kwa kutoonyesha ushirikiano kwa kamati
wakati wa zoezi hilo jambo alilolieleza kuwa limesababisha Kamati kufikisha
malalmiko kwa Mbunge wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli na hatimaye kwa Naibu
Waziri wa Arhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwa lengo la
kupatiwa ufumbuzi
Pepo alisema, kutokana
na Kampuni ya PMM 2001 Ltd kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyokuwa
yatekelezwe Septemba 2018 wamechoka kufuatilia suala hilo na wanachotaka kwa sasa ni wao waliolipwa fedha za awali
kukamilishiwa kiasi kilichopaki na hawako tayari kuendelea na zoezi hilo tena kwa
kuwa kampuni hiyo imeshindwa kuonesha ushirikiano.
Mbunge wa jimbo la
Segerea Bonna Kamoli ameitaka kampuni ya PMM 2001 Ltd kueleza bayana kiasi cha
fedha kilichobaki kwa wamiliki wa nyumba 17 zitalipwa lini lakini Mkurugenzi wa
Fedha na Utumishi wa PMM 2001 Ltd Kanuti alishindwa kutoa jibu na kutaka
kampuni yake kupewa muda kulifanyia kazi suala hilo.
No comments:
Post a Comment