HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 15, 2019

MLIMA KILIMANJARO WATUMIKA KATIKA MAPAMBANO VITA DHIDI YA UKIMWI

 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla  akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro  Mhe. Anna Mgwira wakati wa kuwaaga  waendesha baiskeli na  wapanda mlima na waendesha baiskeli 60 wanaoshiriki  kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro 2019 yenye lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro. PICHA/ WIZARA YA MALIASILI NA UTALII.
 Waendesha baiskeli wakijiandaa kupanda mlima Kilimanjaro kuelekea kilele cha Uhuru kiupitia Kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge mwaka 2019 yenye lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro.
  Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla  akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro  Mhe. Anna Mgwira wakati wa kuwaaga  waendesha baiskeli na  wapanda mlima na waendesha baiskeli 60 wanaoshiriki  kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro 2019 yenye lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwaongoza wapanda  mlima Kilimanjaro 32 walioanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa siku 7 kupitia kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro 2019. Kampeni hiyo ina  lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.  Dkt. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi Bendera ya Taifa kiongozi wa timu ya waendesha baiskeli 28, Bw. Paul Pulson wakati wa kuwaaga waendesha baiskeli hao kutoka mataifa mbalimbali kupitia kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro 2019 yenye lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi na kuchangisha kwa ajili ya watoto yatima na wanaoishi na VVU, leo mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi Bendera ya Taifa kiongozi wa timu ya wapanda mlima Kilimanjaro 32 Bw. Moses Rusasa wakati wa kuwaaga wapanda mlima hao kutoka mataifa mbalimbali kupitia kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro 2019 yenye lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, leo mkoani Kilimanjaro.


WMU, Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amepongeza juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali kutangaza utalii na uanzishwaji wa kampeni zinazohamasisha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kupitia vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.

 Dkt. Kigwangalla ametoa pongezi hizo leo mkoani Kilimanjaro wakati wa hafla fupi ya kuwaaga Wapanda mlima 32 na Waendesha Baskeli 28 kutoka nchi mbalimbali walioshiriki kupanda mlima Kilimanjaro kupitia Kampeni ya Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019 inayolenga kukusanya fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi na kuwasaidia watoto yatima. 

Amesema kampeni hiyo itawawezesha wapanda mlima hao kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak) na waendesha Baiskeli kuzunguka mlima Kilimanjaro takribani Kilometa 500 ikiwa ni sehemu ya kushiriki katika changamoto ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika mwitikio dhidi ya VVU na Ukimwi.

“Ugonjwa wa UKIMWI umeendelea kuwa suala la kipaumbele kwa Serikali, athari zake zinagusa sekta zote ikiwemo wizara ninayoiongoza ya Maliasili na Utalii, bila shaka sote tumeona jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kupambana na janga hili” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.

Amesema kuwa pamoja na takwimu kuonesha kupungua kwa maambukizo mapya bado jitihada zaidi zinahitajika ili kuutokomeza ugonjwa huo akifafanua  kwamba kila mwananchi ni lazima awe macho kuhakikisha anashiriki kutokomeza ongezeko la maambukizo mapya.

Aidha, amefafanua kuwa programu hiyo imetoa mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Mlima Kilimanjaro wakati na baada ya msimu wa Kill Challenge kumalizika kwani wageni kutoka ndani nan je ya Tanzania huwataarifu wenzao pindi wanaporudi makwao ili waweze kuja kupanda mlima Kilimanjaro.

“Huu ni uthibitisho tosha kwamba programu hii siyo tu inachangia kudhibiti Ukimwi bali pia inachangia kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia mapato ya utalii ya Mlima Kilimanjaro” Amesema.

Dkt. Kigwangalla ameipongeza kampuni ya GGL na wawekezaji wote ambao wamekua wakijitoa kuchangia ustawi wa jamii ya watanzania akitoa wito kwa makampuni mengine kuendelea kujitolea kuchangia program hiyo pamoja na Mfuko wa hisani wa UKIMWI ulioanzishwa na Serikali wa AIDS Trust Fund (ATF).

 Amesema hatua ya GGL kushirikiana na Serikali kupitia TACAIDS ni ya kupigiwa mfano na kwamba inaonesha namna sekta binafsi hususani wafanyabiashara wanavyoendelea kujitokeza kuchangia mwaka hadi mwaka.

Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa program hiyo takribani shilingi bilioni 13 za Kitanzania zimekusanywa kupitia jitihada hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko amewapongeza wadau wote kwa kuendelea kuchangia kwenye Mfuko wa kupambana na Ukimwi.

Amesema kuwa mujibu wa takwimu zilizopo TACAIDS ugonjwa wa UKIMWI bado ni tatizo nchini kutokana na kuwepo kwa maambukizi mapya ya watu 200 kila siku.
Amesema kazi kubwa inayofanywa na TACAIDS kwa sasa ni kuendeleza kampeni ya kuzuia maambukizi yasitokee ili kuendana na makubaliano ya umoja wa Mataifa ya kufikia maambukizo 0 ifikapo mwaka 2030.

“ Bado tunayo kazi kubwa sana ya kuzuia maambukizi haya, watu 200 kwa siku kuambukizwa VVU ni wengi, tunaendelea kujitahidi na kufanya kazi kubwa ya kuelimisha wananchi na kama ingekua ni ajali ingekua ni watu 200 wanaumia kila siku, tunazungumza hizi takwimu kujikumbusha kwamba Ukimwi bado upo” Amesisitiza Dkt. Maboko.

Ameeleza kuwa kiwango cha maambukizi  hayo kinazidi kuongezeka miongoni mwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24  akifafanua kwamba kwamba kati ya watu 200 waliopata maambukizi , watu 80 ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.

“Kwa ujumla maambukizi mapya  yanazidi kushuka isipokuwa kwa vijana yanazidi kupanda juu, sisi kama Tume kwa kushirikiana na wadau tunaliona na tunaendelea kulifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kunusuru kizazi cha vijana ambao ndilo tegemeo la Taifa na viongozi wa baadae” Amesisitiza Dk. Maboko.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Mhe. Oscar Mukasa amesema kuwa kazi yao kama Kamati ni kushirikiana na wadau wote katika masuala ya  Sera, Sheria na usimamizi na kufafanua  kuwa mfuko wa Ukimwi tangu kuanzishwa kwake umekuwa na changamoto ya kupata fedha akiupongeza Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kuendelea kuchangia fedha katika mfuko huo.

Amesema Bunge itaendelea kuishauri Serikali kwa lengo la kupata vyanzo vingine vya mapato vya uhakika ili Serikali iweze kushirikiana na wadau wa ndani wa Sekta binafsi kwa lengo la kujitegemea.

Amesema tukio hilo la wapanda mlima kuchangisha fedha linapeleka ujumbe kwa jamii kwamba kazi ya kupambana na UKIMWI bado ni kubwa na endelevu hivyo jamii yote inapswa kushiriki kikamilifu.

No comments:

Post a Comment

Pages