Na Janeth Jovin
MAHAKAMA
Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi,
imemtia hatiani raia wa Nigeria Christian Ugbechi baada ya kumkuta na
hatia ya kusafirisha pipi 56 za dawa za kulevya aina ya heroin
hydrochloride.
Uamuzi huo
umefikiwa leo na Jaji Sirrilius Matupa ambae amesema upande wa
mashitaka katika kesi hiyo umeweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka
kupitia mashahidi wake 11 na vielelezo 22 waliofika mahakamani hapo
kuthibitisha mashitaka hayo, kuwa mshitakiwa ametenda kosa hilo.
Amesema
pamoja na mshtakiwa kujitetea kwamba alifanyiwa upekuzi mara tatu na
hakukutwa na kitu chochote, upande wa mashitaka ulipaswa kuleta
ushahidi wa CCTV na kuongeza kuwa haikuwa lazima kuwapangia upande huo
wa mashitaka mashahidi wa kuwaleta na kwamba walikuwepo mashahidi
wengine waliothibitisha mashitaka.
Amesema
Mkemia Mkuu wa serikali katika uchunguzi wake, amethibitisha dawa za
kulevya alizozichunguza ndizo alizokutwa nazo mshitakiwa huyo.
Kabla
ya kusomwa kwa adhabu Jaji Matupa aliuliza upande wa mashtaka kama
walikuwa na lolote la kusema ambapo Wakili wa Serikali, Constantine
Kakula amedai kuwa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshitakiwa
lakini wameiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Upande
wa utetezi, Jeremiah Ntobesya aliomba mahakama kumpunguzia adhabu mteja
wake kwa sababu ana mke na watoto wawili wanaomtegemea na pia mshtakiwa
anasumbuliwa na matatizo ya moyo na kwamba amekaa gerezani kwa mwaka
mmoja na nusu ambapo katika kipindi hicho chote alikuwa na tabia njema.
Pia
alisema, pamoja na kwamba kifungu cha sheria kinaamuru mshtakiwa
kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani lakini siyo lazima, itolewe
adhabu hiyo, mahakama inaweza kuamua vinginevyo.
Kutokana
na ubishani wa kisheria juu ya adhabu anayopaswa kusomewa mshitakiwa
mahakama imesema itamsomea mshitakiwa huyo adhabu yake, Juni 21, 2019
(Ijumaa).
Mapema
katika ushahidi wake, askari wa upelelezi kutoka Kituo cha Uwanja wa
ndege namba G 1782 D/C Peter alidai kuwa aliandika maelezo ya mshitakiwa
huyo na katika mahojiano alimueleza kuwa amemeza pipi za dawa za
kulevya.
Alidai baada ya
kueleza hayo alimuweka mahabusu ili aweze kuzitoa na kwamba hadi
Januari 30,2018 saa 10:30 jioni alitoa pipi 23 alizomeza.
Pia
alidai walichukua kielelezo hicho na pipi nyingine zilizokutwa kwenye
begi na kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa serikali ambapo kwa pamoja
zilikutwa na uzito wa gramu 947.17.
"Matokeo
ya uchunguzi yalionesha kuwa pipi zote zilikuwa ni dawa za kulevya
ambazo ni heroin hydrochloride zilizochanganywa na paracetamol
metronidazole na papavirine," alidai Peter.
Mkuu
wa Kituo cha Uwanja wa ndege, Inspekta Dickson Haule alidai siku ya
tukio majira ya saa 14:00 mchana akiwa ofisini alijulishwa na askari
huyo wa upelelezi kuwa kuna mtuhumiwa amekamatwa na dawa za kulevya.
Haule
alidai baada ya taarifa hiyo alienda Ofisi ya Polisi Interpol
walipokuwa na alishuhudia mtuhumiwa akipekuliwa ndipo aliona begi dogo
la mgongoni kuna pipi 56 zikiwa zimeviringishwa ndani ya soksi mbili
nyeusi.
Katika kesi hiyo,
inadaiwa Januari 28, mwaka jana maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere (JNIA) wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa
akisafirisha sha dawa za kulevya aina ya Heroine hydrochloride zenye
uzito wa gramu 947.57.
No comments:
Post a Comment