HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 18, 2019

Wadau wa kilimo wampongeza JPM kwa kutaka TADB iwe na matawi mikoani

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine. 


Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
                        
Wadau wa Kilimo wamepongeza pendekezo la Rais John Magufuli la kutaka Benki ya Maendeleo ya kilimo(TADB) kuwa na matawi mikoani ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na huduma nyingine za benki hiyo.

Rais alitoa pendekezo hilo alipokutana na wafanyabishara kutoka nchi nzima juma lililopita Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Wadau wamesifu pendekezo la rais kwa kusema benki hiyo ikiwa karibu na wateja wake na kutoa mikopo kwa wakati, jambo hilo litachochea kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi hapa nchini. Wamesema TADB ipo katika nafasi nzuri ya kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta ya kilimo jambo ambalo linahimizwa sana na rais.

Akihojiwa juu ya maoni ya wadau wa benki yake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw.Japhet Justine, amesema Benki inayafanyia kazi kimkakati maelekezo ya rais na kufafanua kwamba tayari ofisi zimefunguliwa katika baadhi ya mikoa.

Ameeleza kwamba tayari ofisi zimefunguliwa katika mji wa Kigoma na majiji ya Mwanza na Dodoma.

Ofisi ya Mwanza, ameeleza, ilifunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tarehe 19 Machi, mwaka huu na inahudumia  mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera.  

Maandalizi ya mwisho yanafanywa kufungua ofisi katika Jiji la Mbeya, ameeleza kiongozi huyo, na kufafanua kwamba ofisi hiyo itahudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, na Ruvuma.

Ofisi ya Dodoma, amaeleza, imefunguliwa toka mwaka jana na ofisi ya Kigoma imekuwa ikuhudumia wakulima kwa mieze tisa iliyopita.

“Tunafarijika wadau wanapoeleza uhitaji wa huduma zetu na kutambua kazi yetu.  Agizo la rais linaimarisha  dhamira yetu ya kuwa karibu na wananchi na linatupa hamasa ya kufungua ofisi mpya za kongani ili kuhudumia wateja wetu,” ameeleza Bw Justine.

“Kama ulimsikiliza vizuri, Rais Magufuli ameonyesha kuguswa na utendaji kazi wa Benki ya Kilimo na ndiyo sababu anapenda ifungue matawi mikoani ili kusaidia  serikali ya awamu ya tano kuharakisha azima yake ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo 2025. Ujenzi wa viwanda msingi wake mkuu ni kilimo, mifugo na uvuvi,” amesema Bw.Anangisye Mwakalindile,  mkulima wa Parachichi wa Wilaya ya Rungwe,  Mkoani Mbeya.

Bw Mwakalindile amekumbusha pia kwamba  wakati akiwa katika ziara Mkoani Mbeya, Rais Magufuli  aliwaasa wakulima  kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Benki ya Kilimo ili kukuza mitaji na kuinua kilimo nchini.

Bw.Samson Maduhu,  Mkulima wa Pamba, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza amesema TADB  ikiwa na matawi mikoani  wakulima  watanufaika na  mikopo kwa kuongeza tija katika kilimo.

“Mimi nipo kwenye nafasi nzuri ya kuelezea umuhimu na faida ya kuwepo kwa Benki hii kwani katika kipindi kifupi wakulima wengi wa pamba tumenufaika na huduma za benki  hiyo kwa kupata pembejeo mbalimbali kwa urahisi na kwa wakati,” amesema Bw. Maduhu.

Bw.Evodius Barongo, mfanyabiashara wa  kahawa wa Wilaya ya Ngara,  Mkoani Kagera amesema Wanakagera wengi wameona umuhimu wa Benki ya Kilimo kupitia vyama vya ushirika.  Benki imetoa  mikopo ya zaidi ya bilioni 32 katika kwa ajili ya kukuza zao la kahawa.

 Serikali ya Awamu ya Tano inataka Tanzania ijenge uchumi wa kati wezeshi na unaoategemea viwanda ifikapo 2025.

Katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja TADB imerejesha matumaini kwa wadau wa kilimo nchini kwa kuwapatia mikopo  ambayo imesaidia kuinua hali ya wakulima  na kukuza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages