Kaimu
Mkurugenzi, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin
Msiangi akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael kufungua kikao
kazi cha siku tatu cha Watunza Kumbukumbu na Maafisa Rasilimaliwatu
Serikalini chenye lengo la kujadili masuala ya utunzaji wa kumbukumbu na
nyaraka katika Utumishi wa Umma kilichoanza leo jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akisisitiza jambo alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku tatu cha Watunza Kumbukumbu na Maafisa Rasilimaliwatu Serikalini chenye lengo la kujadili masuala ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika Utumishi wa Umma kilichoanza leo jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akifungua kikao kazi cha siku tatu cha Watunza Kumbukumbu na Maafisa Rasilimaliwatu Serikalini chenye lengo la kujadili masuala ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika Utumishi wa Umma kilichoanza leo jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imewataka Watunza
Kumbukumbu na Maafisa Rasilimaliwatu kuhakikisha kumbukumbu na nyaraka zinatunzwa
vizuri kwa kuzingatia uadilifu, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na
Serikali ili kurahisisha utendaji kazi.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis
Michael alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku tatu cha Watunza Kumbukumbu na
Maafisa Rasilimaliwatu Serikalini chenye lengo la kujadili masuala ya utunzaji
wa kumbukumbu na nyaraka katika Utumishi wa Umma kilichoanza leo jijini Dodoma.
Dkt. Michael amesema, uadilifu
katika kutekeleza majukumu yetu ni jambo la msingi sana hivyo kwa wale ambao si
waadilifu wabadilike ili tuweze kuwa na mchango katika kujenga utumishi wa umma
uliotukuka.
Dkt. Michael amefafanua kuwa,
kukosekana kwa taarifa sahihi na kwa wakati kunaweza kufanya Watendaji wa
Serikali kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kusababisha
ucheleweshwaji wa maamuzi au kutolewa kwa maamuzi yasiyo sahihi na yasiyokidhi
matarajio ya wananchi.
“Kutotunza vizuri kumbukumbu na
nyaraka, mianya ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na matumizi mabaya ya
madaraka kunachangia sana kuzorotesha maendeleo ya uchumi wa Taifa.” Dkt.
Michael ameongeza.
Sanjari na hayo, Dkt. Michael
ameipongeza Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kwa kuandaa kikao kazi
hicho na ameitaka Idara hiyo kuhakikisha kinakuwa endelevu ili kuongeza elimu
ya utunzaji kumbukumbu ambao kwasasa unalenga kuboresha uendeshaji wa Masijala
kutoka kwenye mfumo wa kawaida kuwa wa kielektroniki.
Aidha, Dkt. Michael amesema Serikali
itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali za kada ya Watunza Kumbukumbu
kadri zinavyojitokeza ili kuboresha utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za
Serikali.
Naye Kaimu Mkurugenzi, Idara ya
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi ameahidi kufanyia kazi
maelekezo yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu ili utunzaji wa kumbukumbu na
nyaraka katika taasisi za umma uwe na manufaa katika utendaji kazi wa taasisi
na kwa maendeleo ya taifa.
Bw.
Msiangi amesema kikao kazi hicho kimeongozwa na Kauli Mbiu isemayo ni “Utoaji
wa Huduma za Masijala katika Mifumo ya Kielektroniki:Wajibu wetu na Utunzaji
bora wa Kumbukumbu katika kuimarisha utoaji huduma Serikalini.”
Mada zinazojadiliwa ni pamoja na Utunzaji na Utumiaji wa Kumbukumbu katika Utumishi wa Umma, Kumbukumbu za Mahakama na Umuhimu wake katika Kutenda Haki kwa Wakati, Matumizi ya TEHAMA katika Uendeshaji wa Masijali za Serikali.
Mada nyingine ni Wajibu, Usalama na Usimamizi wa Utunzaji Kumbukumbu Tuli katika Taasisi za Umma, Ukusanyaji wa Nyaraka kutoka Taasisi za Umma katika Kuhifadhi Historia na Urithi Andishi wa Taifa letu na Uzingativu wa Maadili katika Utunzaji wa Kumbukumbu na Taaifa za Serikali.
Kikao kazi hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa na kimeshirikisha Watunza Kumbukumbu na Maafisa Rasilimaliwatu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
No comments:
Post a Comment