Ujumbe
wa washirika wa maendeleo ulitembelea maeneo mbalimbali ya mradi. Pichani ni sehemu
ya eneo la Tiba ya Maji.
Washiriki
wa mkutano wakikagua miundombinu ya tiba ya maji kwenye mradi wa Maji wa
Lamadi. Wa kwanza ni Mratibu mradi wa LV WATSAN kutoka EIB, Raoul Pedrazzani.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Serikali imesema
imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa maji wa Lamadi uliopo Wilaya ya
Busega Mkoani Simiyu ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 93.
Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Mhandisi Emmanuel Kalobelo alisema hayo hivi karibuni wakati wa
ziara yake kwenye mradi huo.
Katika ziara hiyo
Mhandisi Kalobelo alifuatana na washirika wa maendeleo wanaowezesha utekelezaji
wa miradi ya maji kupitia Programu ya Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi
wa Mazingira ijulikanayo kama LV WATSAN ambao ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya
(EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
Mhandisi Kalobelo
alisema amefarijika kushuhudia hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi na
aliongeza kuwa hadi kufikia Agosti mwaka huu utakuwa umekamilika kwani shughuli
iliyopo kwa sasa ni ya ufungaji wa pampu na baada ya hapo maji yataanza kutoka.
Kwa upande wake Mratibu
mradi kutoka EIB, Raoul Pedrazzani alisema miradi inayotekelezwa chini ya
Programu ya LV WATSAN imeonyesha mafanikio makubwa na aliipongeza Mamlaka ya
Maji Mwanza (MWAUWASA) ambayo inajukumu la kusimamia miradi hiyo kwa niaba ya
Wizara ya Maji kwa usimamizi mahiri wa utekelezaji wake.
Pedrazzani alisema EIB
ina nia ya dhati ya kupanua ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika siku
zijazo kwani imeridhishwa na namna ambavyo Serikali inatekeleza miradi maeneo
mbalimbali kote nchini.
Naye Afisa Miradi
kutoka AFD, Clement Kivegalo akizungumza kwa niaba ya ujumbe alioambatana nao,
alisema wameridhishwa na hatua ya utekelezaji wa mradi na kwamba AFD itaongeza
udhamini kadri itakavyohitajika kufanya hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Busega, Tano Mwera ambaye alikuwa mwenyeji wa ugeni huo wilayani
hapo, alisema mradi unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwenye wilaya na hususan
katika mji wa Lamadi na alitoa wito kwa wawekezaji kujitokeza kwani maji ya
yhakika yamepatikana na kwamba miundombinu mingine ipo vizuri ikiwemo barabara
na umeme wa uhakika.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga akiuelezea mradi alisema
unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia
moja kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka EIB na AFD kwa gharama ya Shilingi
Bilioni 12.83.
Mhandisi Sanga alisema
mradi utazalisha lita Milioni 3.3 za maji kwa siku ambayo ni mara mbili ya
mahitaji ya sasa ya wananchi wa Lamadi na maeneo jirani hasa ikizingatiwa
kwamba mradi umebuniwa kuhudumia wananchi zaidi ya 60,000.
Aliongeza kuwa hatua ya
kwanza ya maunganisho kwa wananchi; mradi utaunganisha kaya zipatazo 5000 na
aliwataka wananchi kuchangamkia mradi ili kujiletea maendeleo.
Kabla ya ziara hiyo,
washirika hao wa maendeleo walifanya mkutano Jijini Mwanza na watendaji kutoka
Serikalini kwa ajili ya majadiliano na tathmni ya hatua za zilizofikiwa kwenye
ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa chini ya Program ya LV WATSAN.
No comments:
Post a Comment