Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua jengo la TAKWIMU jijini Dodoma,
Juni 29 2019. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma Mjini, Patrobas Katambi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa
wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mkunda, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt Ashatu Kijaji, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa na
kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu) Andrew Massawe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kaya zinazoishi
kwenye makazi bora zimeongezeka kwa asilimia 16 katika kipindi cha miaka sita
ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2011/2012.
“Kaya zinazoishi kwenye nyumba zenye paa la kisasa zilizoezekwa kwa bati
zimeongezeka kutoka asilimia 68 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 84 mwaka
2017/2018 wakati kuta za kudumu zimeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2011/2012
hadi kufikia asilimia 79 mwaka 2017/2018,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumamosi, Juni 29, 2019) wakati akizungumza na viongozi na wananchi mara baada ya kuzindua Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu lililoko
Makulu, Manispaa ya Jiji la Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Dkt.
John Pombe Magufuli, pia
alizindua ripoti ya matokeo
ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi Tanzania
Bara ya mwaka 2017/18.
Waziri
Mkuu alisema takwimu hizo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu na zinaonyesha jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kujenga
Tanzania ya Viwanda zinaendelea kuwanufaisha wananchi kwa zinagusa moja kwa
moja katika sekta ya ujenzi kama vile viwanda vya saruji, mabati, nondo, na
vinginevyo.
Waziri
Mkuu alisema lengo la Serikali ni kuona
kila Mtanzania anaishi kwenye makazi bora kwani makazi bora huimarisha afya za
wakazi na afya bora ni mtaji wa msingi kwa kila mwanadamu kwa kufanya kazi na
hivyo kukuza uchumi.
“Tuendelee kuunga mkono jitihada za Serikali kuhamasisha wawekezaji wa
ndani na nje waje wawekeze kwenye viwanda vya saruji, mabati, na marumaru ili kuongeza
uzalishaji na kuleta ushindani wa bei ambao utawanufaisha watu wengi na
kuwapatia fursa za kujenga makazi bora ya kuishi,” alisema.
Waziri Mkuu alisema mbali na makazi bora, utafiti huo umebainisha uwepo wa
ongezeko la kaya zilizounganishwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa kutoka asilimia
18 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 29.1 mwaka 2017/2018. “Jitihada za
Serikali chini ya Mpango wa Umeme Vijijini (REA), zinaendelea na utekelezaji wa
Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu wa kusambaza nishati vijijini unaojumuisha vijiji
7,873 katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara ambao unatekelezwa kwa
kipindi cha miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2016/17 na unategemewa kukamilika
mwaka 2020/2021,” alisema.
Akizungumzia hali ya umaskini barani Afrika, Waziri Mkuu alisema kiwango cha umaskini wa kipato
cha Watanzania hakitofautiani sana na nchi nyingine ndani ya bara hilo. “Tukiangalia
hali ya umaskini katika nchi nyingine za Bara la Afrika kwa miaka ya hivi
karibuni, nikianza na Kenya kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi ni
asilimia 36.8 (mwaka 2015), Afrika ya Kusini asilimia 55.5 (mwaka 2015), Rwanda
asilimia 38.2 (mwaka 2016), Zambia asilimia 54.4 (mwaka 2015), Ethiopia asilimia
23.5 (mwaka 2015) na Zimbabwe asilimia 72.3,” alisema.
Alisema kupunguza umaskini kwa
nchi yoyote ile kunapaswa kuhusishwa na uwekezaji kwenye sekta nyingine za kiuchumi
ambazo hugusa na kuwanufaisha wananchi walio wengi. “Nitumie fursa hii kusisitiza kuwa umaskini ni
changamoto kwa dunia nzima na hasa kwa nchi zinazoendelea. Nchi zilizo na hali
mbaya zaidi ni zile zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara kama takwimu rasmi
zinavyoonesha.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ni lazima Serikali iimarishe
upatikanaji wa takwimu kwa kuajiri maafisa takwimu wanaowajibika moja kwa moja
na Ofisi ya Taifa ya Takwimu badala ya kumtegemea mtu anayewajibika kwa
Mkurugenzi wa Halmashauri.
“Leo hii hatuna Afisa Takwimu katika kila Halmashauri, na matokeo yake
hatuna mfumo mzuri wa kupata taarifa kuanzia ngazi ya chini. Tuweke utaratibu
ili hawa watu wawepo na kila Afisa takwimu awajibike kupeleka taarifa yake kwa
Mtakwimu Mkuu kila wakati.”
“Nilipokuwa Naibu Waziri TAMISEMI ninayeshughulikia elimu, nikiagiza
takwimu fulani, kuzipata ilikuwa inachukua zaidi ya wiki mbili, na hiyo ni kwa
Halmshauri moja tu. Na wakati mwingine, taarifa inakujia wakati umeshasahau
kuwa ulitoa agizo uletewe.”
Mapema, akitoa taarifa juu ya utafiti huo, Mtakwimu Mkuu
wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani
ambazo kiwango cha umaskini kimeendelea kushuka na kufikia tarakimu moja.
Alisema utafiti huo uliofanywa na ofisi yake kwa kushirikiana na Benki ya
Dunia, baadhi ya balozi na mashirika ya Umoja wa Mataifa ulilenga kupata makadirio
ya viwango vya umaskini ili kufuatilia, kupima na kutathmini mipango mbalimbali
ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Alisema katika utafiti huo, walitumia teknolojia ya kisasa iitwayo survey solution ambayo imesaidia kupunguza
gharama za utafiti za kupeleka madodoso na magari. “Tulitumia vishkwambi
(tablets) na kupunguza mzigo wa kubeba na makaratasi au kukaa kujumlisha
taarifa,” alisema.
No comments:
Post a Comment