Katibu Mkuu wa Chama
cha Mapinduzi Dk. Bashiru Ally akizungumza na wana CCM katika mkutano Mkuu wa Jimbo la Ilemela tarehe
30 Julai 2019 kuelezea utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kama
ilivyoahidiwa na Mbunge wa Jimbo hilo wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka
2015.
Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Katibu Mkuu wa Chama
cha Mapinduzi Dkt Bashiru Ally amesema hatashangaa kuona mbunge wa jimbo la
Ilemela ambaye ni Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula akipita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu ujao 2020 kutokana
na kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake.
Dkt Bashiru alisema
hayo tarehe 30 Julai 2019 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika
mkutano Mkuu wa Jimbo la Ilemela kuelezea utekelezaji wa ilani ya Chama cha
Mapinduzi kama ilivyoahidiwa na Mbunge wa Jimbo hilo wakati wa kampeni za
uchaguzi za mwaka 2015.
Katibu Mkuu huyo wa
Chama cha Mapinduzi alisema hakuna kumnadi tena Dkt Angeline Mabula kwa kuwa
anazo sifa zinazomuwezesha kutetea kiti chake na yeyote anayetaka kuwania
nafasi katika jimbo hilo ajue kiti hicho kishakaliwa pamoja na kata zake 19.
‘’Ole wake anayetaka
kupita mlango wa nyuma, chama kina utulivu sitashangaa Dkt Mabula akipita bila
kupingwa ‘’ alisema Dkt Bashiru.
Alionya Wabunge wa CCM
waliozembea kufanya ziara za kutatua kero za wananchi pamoja na kufanya vikao kwenye majimbo yao
kuwa hawatakuwa na ulinzi wakati wa kinyanganyiro cha kupendekeza majina ya
kuwania nafasi hizo na kusisitiza kuwa kipaumbele kitatolewa kwa
wabunge waliokuwa wakichapa kazi.
Aliwaaambia wana
Ilemela kuwa, kuna tofauti kubwa sana ya kimaendeleo wakati jimbo la Ilemela lilipokuwa
chini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na sasa linavyoshikiliwa
na Chama cha Mapinduzi.
Kwa upande wake Mbunge
wa Jimbo la Ilemela ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Mabula alisema jimbo lake kwa sasa limepiga hatua kubwa kimaendeleo
katika sekta za elimu, Afya, Maji, Mindombinu, Uzalishaji na Mifugo, Viwanda na
Biashara pamoja na Utamaduni na Michezo ukilinganisha na miaka iliyopita.
Akielezea maendeleo
katika sekta ya Afya ndani ya jimbo hilo, Dkt Mabula alisema jimbo la Ilemela
limefanikiwa kujenga zahanati mbili mpya alizozitaja kuwa ni Buganda na Lukobe,
hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya vya Lumala na Nyamazogo.
Aidha, Mbunge huyo wa
Ilemela alisema katika sekta ya elimu walifanikiwa kujenga shule mpya za
sekondari za Kayenze, Angeline Mabula na Kisundi huku shule za msingi
zikijengwa mbili za Kayenze ndogo pamoja na Ihalalo aliyoielezea kuwa ilijengwa
kwa ushirikiano na serikali ya Korea kusini aliyoiita shule ya mfano na
kubainisha kuwa wilaya ya Ilemela iliongoza kimkoa katika elimu huku ikishika
nafasi ya sita katika kanda ya ziwa.
Akigeukia suala la
migogoro ya ardhi katika jimbo lake ambapo yeye ni Naibu Waziri mwenye dhamana,
alisema jimbo hilo lilikuwa na migogoro mikubwa ya ardhi kati ya wananchi na
jeshi la polisi katika eneo la Kigoto, Jeshi la Wananchi na wakazi wa Nyagugulu
na mgogoro uliohusisha wananchi wa Bwiru ambapo alieleza kuwa migogoro hiyo
sasa imekwisha baada ya wananchi kupatiwa maeneo na wengine kulipwa fidia.
Katika
hatua nyingine Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt
Bashiru Ally ameonya dhidi ya wafanyabiashara wanaotumia lumbesa na vipimo visivyokubalika
katika kupima mazao ya kilimo kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao na
kuwataka wakuu wa mikoa, wilaya na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha
wanasimamia suala hilo kwani utekelezaji wake umeonekana kusuasua.
Alisema, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli alishatoa maagizo kwake
na Waziri Mkuu juu ya suala hilo na
kubainisha kuwa watendaji wa serikali wanapaswa kulisimamia hilo na kusisistiza
kuwa iwe Ushirika ama mtu binafsi matumizi ya vipimo visivyozingatia taratibu
hayakubaliki na mtu wa kutoa taarifa ya matumizi yasiyofaa ya mizani ni
wananchi kupitia CCM.
No comments:
Post a Comment