Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolijia, William Ole Nasha, akiwa katika banda la COSTECH kwenye Monesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba'.
Mkurugenzi Mkuu COSTECH, Amos Nungu, akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo katika viwanja vya Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF).
Mkurugenzi Mkuu COSTECH, Amos Nungu, akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo katika viwanja vya Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF).
Na Tatu Mohamed, Dar es Salaam
NAIBU
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetoa
Sh. Milioni 700 kwa wabunifu 60 ili kuendeleza tafiti na bunifu zao na
kuleta tija na manufaa kwa Taifa.
Akizungumza
leo Julai 10, 2019 wakati wa kongamano maalum la Ubunifu lililoandaliwa
na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kwa
kushirikiana na COSTECH katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa
Dar es Salaam (DITF), Ole Nasha amesema Serikali itaendelea kuwatambua
wabunifu na wagunduzi wa kazi mbalimbali nchini.
Amesema
kwa sasa wapo Watanzania wengi wanaofanya kazi za ugunduzi na bunifu za
kazi mbalimbali lakini zimeshindwa kutambulika na hivyo kuilazimu
serikali kuanza kuweka utaratibu maalum ikiwemo kuandaa mwongozo
unaotarajiwa kuwatambua wabunifu hao katika ngazi mbalimbali.
“Mwaka
jana tuliandaa mashindano maalum ya ubunifu na walipatikana washindi wa
kitaifa 60, kwa kutambua umuhimu wa kazi zao, pamoja na kutoa fedha pia
tumeanza mchakato wa kutoa mwongozo maalum wenye utaratibu wa kuendesha
vituo vya teknolojia na ubunifu,” amesema Ole Nasha.
Aidha
Ole Nasha ameitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuandaa kongamano la
kila mwaka kwa ajili ya kuwakutanisha wafanyabiashara na wabunifu hao
kwa ajili ya kupokea maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa kuwa
hatua hiyo itasaidia kubaini kazi mbalimbali za wabunifu na watafiti na
kuweza kutambulika.
Kwa
mujibu wa Ole Nasha amesema wabunifu na wagunduzi nchini kutambua kuwa
masuala ya ubunifu hayana kiwango cha elimu na kuwataka wabunifu wasio
katika sekta rasmi kuendelea kubuni bidhaa na vifaa mbalimbali kwa kuwa
COSTECH si taasisi inayowagusa wasomi peke yao bali wabunifu wote
waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akifafanua
zaidi Ole Nasha amesema kutokana na wabunifu na watafiti wengi
kukabiliwa na changamoto ya kuibiwa kazi zao, aliitaka COSTECH kukaa
pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Makampuni (BRELA) ili
kuhakikisha kuwa wabunifu wanawekewa utaratibu maalum kwa ajili ya
kulinda bunifu zao.
Kwa
upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Tekonolojia, Prof. James Mdoe amesema serikali itaendelea kuzitambua
kazi mbalimbali za wabunifu na wagunduzi nchini ili kuhakikisha kuwa
kunakuwepo na ushirikiano madhubuti kwa ajili ya kutambua na kuendeleza
kazi za ubunifu na ugunduzi nchini.
Mkurugenzi
Mkuu COSTECH, Amos Nungu amesema wataendelea kuwasaidia wabunifu wa
ndani kuwa kuwapa nafasi ya kuonesha, kusikika na kuzielezea kazi zao
katika maonesho mbalimbali.
"Tunajua
wapo wabunifu wengine shida yao si mitaji bali ni kusikika na kuonesha
bidhaa zao, hivyo tunaimani maonesho haya yanawapa fursa wabunifu wetu
kuelezea na kuonesha bidhaa zao, " amesema.
Aidha
Nungu ametoa wito kwa halmashauri zote nchini kutekeleza agizo la
kujenga kumbi za ubunifu katika maeneo yao, jambo litakaloimarisha
upatikanaji wa maarifa na ujuzi mbalimbali kutoka kwa vijana.
Naye
Mbunifu wa Maji taka kutoka Kampuni ya Biocon Africa Ltd, Prof. Karoli
Njau ameitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wabunifu na
wagunduzi wote nchini ili waweze kuonyesha kazi zao na kuhakikisha kuwa
kuna utaratibu mzuri wa kuwapata watoa huduma katika kazi mbalimbali
zinazoweza kupatikana nchini.
Katika
mkutano huo,Wabunifu wawili kutoka mkoani Njombe wamekabidhiwa vyeti
vya kuwatambua ambao Ni John Fute na Rainel Ngailo wakibuni mitambo ya
kuzalisha umeme na kujenga kumbi ya ubunifu kwa ajili ya kutoa mafunzo
ya kibunifu.
No comments:
Post a Comment