Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dk. Phillip
Mpango, akipokea mfano wa hundi
yenye thamani ya shilingi bilioni moja kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Benki ya TPB, Dkt. Edmund Mdolwa
katika hafla ya kupokea gawio
hilo jijini Dodoma. Benki ya Posta
imetoa gawio hilo ikiwa ni faida iliyopatikamna mwaka 2018.
Na Saidina Msangi na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Serikali imepokea gawio la
Shilingi Bilioni 1
kutoka Benki ya Posta Tanzania
(TPB) linalotokana na faida ya uwekezaji wake wa asilimia 83 ya hisa katika Benki hiyo katika mwaka wa fedha
2018/19.
Hafla ya makabidhiano ya Hundi
kifani ya gawio hilo imefanyika jijini Dodoma, kati ya Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) ambaye alipokea kwa niaba ya Serikali, na
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Benki hiyo Dkt. Edmund Mndolwa.
Akizungumza katika hafla hiyo
Dkt. Mpango aliipongeza Benki hiyo
kwa kutoa gawio kwa Serikali, na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika katika
shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.
“Utoaji huu wa gawio ni kiashiria
tosha kwa Serikali kuwa Benki
inazidi kukua na kuwapa moyo watanzania na wawekezaji kuwa TPB inatoa huduma bora katika jamii”,
alisema Dkt. Mpango.
Aliitaka Benki hiyo kuongeza wigo wa utoaji huduma ili kuwafikia wananchi
hususani waishio vijijini pamoja na kutoa elimu kwa wananchi hao kuhusu umuhimu
wa kuweka akiba, kukopa sambamba na kurejesha mikopo kwa wakati.
“Riba katika benki zetu bado ni kubwa taasisi za
fedha zione namna ya kuzipunguza sambamba na kutoa mikopo kwa kuzingatia
kanzidata ya wakopaji ili kuepuka mikopo chechefu.”, alisisitiza Dkt.
Mpango.
Aidha, Dkt. Mpango ameiagiza Benki hiyo
kuendelea kuwapa wanawake kipaumbele
katika upatikanaji wa huduma za fedha na mikopo ili waweze kuendesha shughuli
za maendeleo.
Pia Dkt. Mpango aliiagiza TPB kusimamia uadilifu kwa watumishi wake na
kuwa makini na kutoa taarifa za miamala
yenye mashaka ili kuzuia utakasishaji wa fedha haramu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya TPB Dkt. Edmund
Mndolwa alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya Sh. Bilioni 17.2 kabla ya kodi ambayo Benki yake imeipata katika mwaka wa fedha 2018/19. Pia ameeleza kuwa Benki hiyo
itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi
kwa ujumla.
Aidha, Dkt. Mndolwa aliipongeza Serikali ya
Awamu ya Tano kwa utendaji mzuri ambao umeiwezesha Benki hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na
kuahidi kuendelea kushirikiana nayo ili kukuza uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment