Bingwa wa mbio za baiskeli kwa afya za Tamasha la Majimaji Selebuka, Masunga Duba, kutoka mkoani Simiyu, akimaliza mbio hizo za kilomita 100, zilizofanyika mkoani Ruvuma. (Na Mpiga Picha Wetu).
Mkurugenzi-Mwenza wa Taasisi ya So-Mi, Prof. Julian Murchison kutoka Marekani, akimpongeza baada ya kumvisha medali, bingwa wa mbio za baiskeli kwa afya Tamasha la Majimaji Selebuka, Masunga Duba zilizofanyika jana Julai 20, mwaka huu mkoani Ruvuma.
Mshindi wa mbio za baiskeli kwa afya Tamasha la Majimaji Selebuka 2019,
Masunga Duba kutoka mkoani Simiyu akikabidhiwa kitita chake cha milioni
moja na Mkurugenzi Mwenza wa Taasisi ya So-Mi, Prof. Julian Murchison
ambayo ndiyo waandaji wa tamasha hilo.
Boniphace Masunga aliyeshika nafasi ya pili katika mashindano ya mbio za
baiskeli kwa afya zilizoandaliwa na Tamasha la Majimaji Selebuka mjini
Songea, Ruvuma akimaliza mbio hizo zilizofanyika jana Julai 20, mwaka
huu.
Na Mwandishi Wetu, Songea
MWENDESHA Baiskeli kutoka Simiyu, Masunga Duba, ameendeleza
ubabe katika Tamasha la Majimaji Selebuka 2019 baada ya kutetea ushindi
alioutwaa mwaka jana.
Katika mbio hizo za baiskeli kwa afya zilizoanzia Makumbusho
ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji hadi eneo la Liganga kisha kurejea, ikiwa ni
umbali wa Kilomita 100, Masunga alishinda akitumia saa 2:50.43 akiboresha muda
alioutumia mwaka jana wa saa 2:53.05.
Nafasi ya pili pia ilikwenda mkoani Simiyu kwa Boniphace
Masunga aliyetumia saa 2:51.01 huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Denis Julias
kutoka Arusha saa 3:15.00.
Masunga kwa ushindi huo alijinyakulia kitita cha Sh. Milioni
1 na medali ya dhahabu huku mshindi wa pili Boniphace akilamba Sh. 700,000 na
medali ya fedha wakati mshindi wa tatu Denis akiondoka na Sh. 500,000 na medali
ya shaba.
Mshindi wa nne aliibuka Ombeni Mbilinyi wa Iringa aliyetumia
saa 3:15.03 na kuzawadiwa Sh. 300,000 na medali ya ushiriki huku nafasi ya tano
ikienda kwa Asso Gadas kutoka Dar es Salaam saa 3:15.41 na kujipoza kwa Sh.
100,000 na medali ya ushiriki.
Ipyana Mbogela kutoka Iringa mshindi wa tatu mwaka jana,
aliporomoka hadi nafasi ya sita akitumia saa 3:20.41, nafasi ya saba ikaenda
kwa Kwilasa John wa Manyara saa 3:22.45, wa nane Hagai Sanga saa 3:30.53, Elias
Tala alitumia saa 3:40.11 huku kumi bora ikifungwa na Abdul Kajenje aliyetumia
saa 3:54.22 wote kutoka Mbeya.
Washindi wa sita hadi kumi kila mmoja alipata kifuta jasho
cha Sh. 50,000 na medali za ushiriki.
Tukio hilo la Baiskeli, ndilo lilikuwa la kuhitimisha tamasha
hilo ambalo lilikata utepe Julai 13 kwa mchezo wa Riadha kwenye Uwanja wa
Majimaji mjini hapa.
Akizungumza wakati wa kufunga tamasha la mwaka huu,
Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Songea Mississippi (So-Mi), ambao
ndio waandaaji wa tamasha hilo, Prof. Julian Murchison, alisema lengo la
kuanzishwa kwa tamasha hilo ni kuinua vipaji na fursa mbalimbali mkoani Ruvuma
na ndio maana wamekuwa wakilifanya kila mwaka.
“Tamasha hili tuna malengo mbalimbali, tunataka kuinua vipaji
hususan kwa vijana mkoani Ruvuma, kutoa fursa na pia kujenga mahusiano bora
kati ya mji mkuu wa Ruvuma, Songea na Mississippi ninakotokea…Kupitia mahusiano
haya tunabadilishana mawazo ya kujenga vitu mbalimbali baadaye,” alisema Prof.
Julian.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tamasha hilo, Nathan Mpangala,
alihuzunishwa na wenyeji kutojitokeza mwaka huu kwenye mchezo huo tofauti na
misimu minne toka lianzishwe tamasha hilo.
No comments:
Post a Comment