NA
TIGANYA VINCENT, TABORA
SERIKALI imeziagiza
Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa kuhakikisha zinaharakisha zoezi la
upimaji wa maeneo na mashamba ya wananchi ili waweze kuwapatia hati miliki za
maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa jana
na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula wakati
wa ziara yake katika Wilaya ya Uyui na Nzega mkoani Tabora.
Alisema hatua hiyo
itasaidia kuondoa migogoro baina yao hata Taasisi nyingine za umma na binafsi
kutokana na kukosekana kwa alama zinazoonyesha mipaka ya maeneo.
Mabula alisema sanjari
na upimaji wa maeneo na mashamba ya wananchi ni vema kuwepo na mpango bora wa
matumizi ya ardhi katika vijiji vyote ili kuzuia ujenzi wa makazi holela.
Aidha alizitaka
Halmashauri zote kuhakikisha zinanunua maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli
mbalimbali za maendeleo ikiwemo kutenga maeneo ya ujenzi wa viwanda na huduma
nyingine za kijamii kama vile shule na Hospitali.
“Nunueni maeneo ya
kutosha na kuyapima …ili anapotokea Mwekezaji ni rahisi kuingia naye ubia…pia
hakikishe kila eneo la umma linapimwa na kupata hati ili kuepuka maeneo ya umma
kuvamiwa” alisema.
Naibu Waziri huyo alisema
ununuaji huo wa maeneo ni lazima uzingatia Sheria na makubaliano ya pande mbili
ya mnunuzi na muuzaji.
Mabula alisema eneo la mtu
lisichukuliwe kabla ya kumlipa fidia anayopaswa kulipwa.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri huyo amewataka Wananchi waliouziwa viwanja kuviendelea la sivyo
vitachukuliwa na kuuziwa wengine.
Alisema kuna baadhi ya
wananchi wanauziwa viwanja lakini wanakaa wanavyo kwa kipindi hata cha miaka
mingi bila kufanya chochote jambo ambalo ni kinyume cha Sheria.
No comments:
Post a Comment