HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 02, 2019

KAILIMA ATOA AGIZO ZITO JESHI LA POLISI

  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani kailima, (Wa kwanza kushoto), Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Central (OCS), Kidwadi Karinga (Wa pili kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko, CP Albert Nyamuhanga (Watatu kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi Kitengo Cha Kushughulikia Malalamiko, Rabikira Mushi wakiwa katika Kituo Kkuu (Central) kilichopo Wilaya ya Dodoma Mjini wakiwa kwenye ziara ya Kikazi kituoni hapo. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani kailima, (Wa kwanza kulia), Mkuu wa Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko, CP Albert Nyamuhanga (Wa pili kulia), Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dodoma (RCO), Pipi Kayumba (Wa tatu kushoto), na Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko, Rabikira Mushi wakiwa katika kituo cha Polisi Nkuhungu kilichopo Wilaya ya Dodoma Mjini  wakikagua kitabu cha taarifa za Polisi (RB) walipofanya ziara ya kikazi kituoni hapo. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani kailima, (wa kwanza kushoto), Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Central (OCS), Kidwadi Karinga (wa pili kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko, CP Albert Nyamuhanga (wa tatu kushoto), wakimsikiliza mwananchi aliyekuwa akisubiri huduma katika Kituo Kikuu cha Polisi, Wilaya ya Dodoma Mjini wakati viongozi wao walipofanya ziara ya kikazi kituoni hapo. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)
PICHA 4: Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima (katikati), akitoa maelekezo kwa viongozi wa Polisi na watendaji wakuu wa Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko baada ya kukamilisha ziara ya kikazi Kituo cha Polisi Chang’ombe, Wilaya ya Dodoma Mjini. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).


Na Mwandishi Wetu, MOHA

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima, amelitaka Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kuboresha mazingira ya huduma wanazotoa kwa wananchi.
Alisema ni wajibu wa jeshi hilo kutoa elimu kwa jamii iweze kufahamu hatua za kufuata pindi wanapotaka kuwawekea dhamana ndugu zao waliopo katika vituo vya polisi.
Kailima aliyasema hayo hayo jana alipofanya ziara ya kutembelea vituo vinne vya polisi mkoani Dodoma.

Lengo la ziara hiyo iliyoandaliwa na Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko Ndani ya Wizara hiyo ni kuangalia utendaji kazi wa jeshi hilo juu ya huduma wanazotoa kwa wananchi.

Vituo alivyotembelea ni vile vilivyopo katika Wilaya ya Dodoma Mjini ambavyo ni Kituo Kikuu (Central), Chang’ombe, Nkuhungu na Kikosi cha Usalama Barabarani.

Katika ziara hiyo, Kailima aliambatana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Kushughulikia Malalamiko, Kamishna wa Polisi, Albert Nyamuhanga pamoja na Maafisa wengine wa kitengo hicho.

Akiwa kwenye kituo Kikuu cha Polisi (Central), Kailima alikuta idadi kubwa ya watu waliokuwa na shida mbalimbali, alitumia fursa hiyo kuzungumza nao na kuwataka waeleze kero zao.

Baada ya kuzungumza na wananchi, Kailima aliushauri uongozi wa kituo hicho kuweka mazingira mazuri ya kutoa huduma ili kuondoa mrundikano wa wananchi nje, ndani ya kituo.

“Wekeni mazingira mazuri ya mwananchi mmoja kuhudumiwa na askari mmoja kutokana na idadi ya askari ambao watakuwa zamu ili kupunguza msongamano,” alishauri.

Aliongeza kuwa; “Toeni elimu inayohusu dhamana kwa jamii ili wananchi wajipange kabla ya kuja kituoni, unakuta watu wengi wanakuja kuwawekea dhamana ndugu zao bila kujua taratibu hivyo kusababisha wajazane kituoni bila sababu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Dodoma, Pipi Kayumba, alisema katika utendaji kazi wake, kila siku anapita kituoni hapo ili kuonana na wananchi anaowakuta kituoni, kusikiliza shida zao.

Alishauri ili jeshi hilo liweze kuboresha huduma zake, kuwepo vituo vya polisi katika njia zote za kuingia jijini Dodoma kwani jiji hilo limekuwa kubwa, idadi ya watu imeongezeka.

“Kwa sababu ya ongezeko kubwa la watu, hata utoaji huduma nao umekuwa mkubwa, kuanzishwa kwa vituo hivyo litakuwa jambo jema kwa Jeshi la Polisi na nchi kwa ujumla,” alisema.

Kwa upande wake, Kamishna Nyamuhanga alishauri Mkuu wa Kituo hicho, Kidwadi Karinga, aweke mkakati wa kuondoa malalamiko ya wananchi kwenye kituo hicho.

Kailima aliendelea na ziara yake kwenye Kituo cha Kikosi cha Usalama Barabarani, kuzungumza na wananchi waliodai kuna mtu ambaye si askari  alikuwa akitoa taarifa ya upotevu wa mali (loss report).

Mtu huyo alikuwa akitoa taarifa hiyo nje ya kituo hicho kwa gharama kubwa wakati gharama halisi ni sh. 500 tu, hulipwa kwa utaratibu uliowekwa na kupewa risiti.

Kailima alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa lengo la ziara hiyo ni kujionea mazingira ya kazi za askari kwa jamii ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

Alimpongeza Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Nuru Selemani kwa kutekeleza agizo la Waziri wa Wizara hiyo, Kangi Lugola juu ya kuziondoa pikipiki zilizokamatwa kwa makosa mbalimbali.

“Wasisitize askari wako waache kuomba na kupokea rushwa, kutobambika kesi kwa wananchi, askari kutumia lugha nzuri, kuelimisha wananchi wanapofanya kosa, kutoa elimu katika  redio namna ya kuvuka kwenye zebra, kutoa taarifa kuhusu hali ya mji kila siku,” alisisitiza Kailima.

Aliwataka askari wa Usalama Barabarani wafanye operation kubwa mara moja kwa mwezi ili kufanya wepesi wa kukusanya maduhuli ya serikali, kutimiza wajibu wao wawapo kazini na wanaokwenda tofauti wachukuliwe hatua stahiki.

Alisisitiza suala la usalama hasa kipindi hiki ambacho kuna ugeni wa Mkutano wa SADC kuanzia Agosti 5, mwaka huu, hivyo kama chombo cha usalama wamuunge mkono Rais Dkt. John Magufuli.
Pia Kailima alitembelea Kituo cha Chang’ombe kinachohudumia kata tatu za Chamwino, Chang’ombe na Chinangali ambapo hali ya usalama si nzuri kutokana na matukio ya wizi, unyang’anyi.

Matukio hayo yamelifanya jeshi hilo kufanya msako mkali na tayari baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.
Kailima aliushaurio uongozi wa kituo hicho na askari kuitumia jamii au serikali za mitaa ili kupata taarifa za wahalifu.

Mkuu wa kituo hicho, Emanuel Mawi, alisema kuna doria inafanyika maeneo mbalimbali, pia wanashirikiana na jamii, changamoto waliyonayo ni udogo wa kituo ambacho kinahudumia eneo kubwa.

Akiwa kwenye Kituo cha Nkuhunga, Kailima aliambiwa kituo hicho kinahudumia kata mbili za Nkuhungu na Kizota.
Akiwa kituoni hapo, Kialima aliambiwa kituo hakilazi mahabusu ambao hupelekwa Kituo Kikuu (Central).

Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Dodoma, Kayumba alisema changamoto waliyonayo ni uchache wa magari kwa ajili ya doria za kila siku.

Kailima aliwapongeza Kayumba na Karinga kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Kwa upande wake, Kamishna Nyamuhanga, alimshukuru Kailima na kumuahidi kuwa, watatekeleza maelekezo yote aliyotoa katika ziara hiyo ili kuboresha utendaji kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages