Mbunge
wa Ubungo, Saed Kubenea, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam jana na kuitaka Serikali kuridhia na kusaini Itifaki ya
Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu kuhusu haki za watu wenye ualbino.
Kutoka kushoto ni Mwanasheria wa Under the Same Sun, Kondo Seif, Katibu
wa Chama cha Watu wenye Ualbino Wilaya ya Ubungo, Mwamvua Kambi,
Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino Wilaya ya Ubungo, Mussa Geuza
na Pendo Manoni. (Picha na Francis Dande).
NA
JANETH JOVIN
Mbunge
wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka
kuridhia na kusaini Itifaki ya Mkataba wa Afrika wa haki za binadamu kuhusu
haki za watu wenye ualbino.
Amesema
mkataba huo uliopitishwa mwaka jana katika mkutano wa 30 wa wakuu wa nchi za
Umoja wa Afrika haujasainiwa mpaka sasa,
licha ya kwamba unatambua na kuvisemea vitendo vya mauaji na ukatwaji
viungo kwa watu wenye ualbino barani Afrika.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kubenea alisema atapeleka
hoja binafsi kuitaka serikali kuridhia na kusaini itifaki ya mkataba huo, kwani
watu wenye ualbino nchini ni jamii iliyopo hatarini kufutika kutokana na wengi
wao kuuawa kwa imani za kishirikina.
Alisema
kwa kuwa itifaki ya mkataba huo imetambua mambo hayo yote hivyo
ni muhimu kwa serikali kuridhia na kuisaini haraka, ili ufanye kazi.
“Hata
hivyo Itifaki hii pia imezipa majukumu nchi wanachama kuchukua hatua
madhubuti za kisera, kisheria, kiuongozi, kitaasisi, na kibajeti, ili kukomesha
ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu ingawa Itifaki hii bado haijaridhiwa na
kusainiwa na nchi yetu.
“Kuridhia
na kusainiwa kwa itifaki ya mkataba huu wa Afrika, sio tu kutaonyesha juhudi na
hatua za kimataifa kutangaza dhamira njema ya kudumisha haki na ustawi wa
wananchi wenye ualbino na kundi la watu wenye ulemavu kwa ujumla, bali pia kutaifanya
nchi yetu kuwa mfano wa kuigwa na jumuiya ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ambazo
pia zinakabiliana na changamoto hii,” alisema.
Hata
hivyo Kubenea ameiomba Serikali kufanya marekebisho ya Sera ya Watu wenye
ualbino iliyotungwa mwaka 2004 ili ikidhi mahitaji ya makundi yote.
Mwanasheria
wa Shirika la Kimataifa la Under the Same Sun, Maduu William,
alisema Afrika ndio taifa pekee ambalo watu wake wanaamini, ili wawe matajiri
lazima wapate kiungo au nywele ya mtu mwenye ualbino.
Alisema
ili kuondokana na dhana hiyo, itifaki hiyo inapaswa kuridhiwa na kusainiwa, kwani
inapinga jambo hilo kwa nguvu zote.
Mwenyekiti
wa Chama cha Watu wenye Ualbino Wilaya ya
Ubungo,
Mussa Geuza, aliwaomba wabunge wengine waungane na Kubenea kuwatetea na
kuhakikisha itifaki ya mkataba huo inaridhiwa na kusainiwa na serikali.
No comments:
Post a Comment