HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 12, 2019

Matunda: Njooni mumuone Kolokolo Domorefu

Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mazingira Asili Amani, wilayani Muheza Mkoani Tanga, Bob Matunda akizungumza na waandishi kuhusu vivutio vilivyopo hifadhini hapo. (Picha na Suleiman Msuya).

NA SULEIMAN MSUYA
HIFADHI ya Mazingira Asili ya Amani, Muheza Tanga inawakaribisha Watanzania na wageni kutoka nje kufanya utalii katika hifadhi hiyo ili waweze kujionea viumbe adimu akiwemo Kolokolo Domorefu asiyepatikana kwingine duniani.
Mwaliko huo umetolewa na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Bob Matunda wakati akizungumza na Tanzania Daima hivi karibuni.
Matunda alisema hifadhi hiyo ni moja ya hifadhi ya kipekee duniani na kwamba ina viumbe adimu ambao hawapatikani popote duniani tofauti na hapo.
Alisema hifadhi hiyo inatambulika kama hifadhi ya ndege wa aina mbalimbali huku akipatikana ndege wa kipekee anayejulikana kama Kolokolo Domorefu, mijusi, mau ya Sant Pauline ambayo yanapatikana Tanzania na nchini Ujerumani.
“Naomba kutumia nafasi hii kuwaomba Watanzania na wageni kutoka nje waje waone vivutio vya aina yake ambavyo havipo kokote duninia kama ndege Kolokolo Domorefu ambaye yupo kwenye mradi wa Nature Tanzania ni kivutio ambacho kinatuingizia watalii kutoka duniani kote,” alisema.
Matunda alisema kupitia ndege huyo na viumbe wengine wanaopatikana hifadhini hapo kuanzia mwaka jana hadi sasa wamefanikiwa kupokea watalii na watafiti zaidi ya 1,000 na matarajio yao ni kuongeza idadi.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Nature Tanzania, Victor Mkwongewa, alisema taasisi hiyo imeamua kushirikiana na hifadhi kulinda ndege hao ambao wapo 249 duniani kote pamoja na kuchochea utalii wa ndege ambao unakua kwa kasi duniani.
Mkurugenzi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo alisema shirika lao limejitolea kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wa vijiji ili waweze kulinda viumbe adimu wanaopatikana katika msitu wa Amani.
Lyimo alisema pia wanatoa elimu kwa watoto wa shule za msingi kwa kushirikiana na hifadhi na Nature Tanzania ili kuweza kuwarisisha uhifadhi wa misitu na viimbe vilivyopo kwenye msitu ili viweze kuwa vivutio vya utalii na kuwaingia kipato.

No comments:

Post a Comment

Pages