HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 13, 2019

Prof.Kabudi: Uenyekiti wa Tanzania utachochea viwanda SADC

Mwenyekiti Mpya wa Kamati ya Baraza la Mawaziri, wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Prof. Palamagamba Kabudi, akizungumza baada ya kupokea kijiti cha Uenyekiti kutoka kwa Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Netumbo Ndaitwah ambaye ni Naibu Waziri Mkuu wa Namibia. (Picha na Suleiman Msuya).

NA SULEIMAN MSUYA

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kahudi, amesema  wataitumia nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuchochea kasi ya uanzishwaji viwanda kwa nchi wanachama.

Waziri Kabudi aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam baada ya kupokea kijiti cha Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC kutoka kwa Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Netumbo Ndaitwah ambaye in Naibu Waziri Mkuu wa Namibia.

Waziri Kabudi alisema nchi za SADC zinapaswa kufikia maendeleo kwa kasi hivyo sekta ya viwanda ni njia muhimi kufikia lengo hilo.

Alisema mwaka mmoja wa uongozi wake pamoja na mambo mengine ambayo watayafanya ni lazima kasi iwepo kwenye viwanda.

"Nitahakikisha  nashirikiana na wenzangu katika kamati na viongozi wa nchi kuchochea uanzishwaji wa viwanda kwa nchi wanachama kwani  viwanda ndio chachu ya uchumi na maendeleo," alisema.

Alisema anaamini iwapo kila nchi mwanachama itajikita kwenye uanzishaji wa viwanda na ujenzi wa miundombinu changamoto ya kiuchumi, ajira na huduma za jamii.

Mwenyekiti huyo mpya wa Kamati ya Baraza la Mawaziri wa SADC, alisema umaskini uliokidhiri kwa nchi wanachama na Afrika kwa ujumla unachangiwa na kukosekana uwekezaji kwenye sekta muhimu kama viwanda.

Aidha, alisema katika uongozi wao watapigania lugha ya kiswahili kutumika kama lugha rasmi ya SADC kwani Tanzania ina mchango mkubwa kwa jumuiya hiyo.

Alisema pia watajikita kupigania vikwazo vya kibiashara iliyowekewa nchi ya Zimbabwe vinaondolewa ili kuchochea maendeleo.

"Lakini pia tutasimamia haki za watoto, wanawake na jamii kwa ujumla kwani hatutaki kumuacha mtu nyuma ndani ya jumuiya," alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Ndaitwah alisema nchi wanachama zinufaike na SADC ni lazima zisimamie utekelezwaji wa Eneo Huru la Biashara (FRA).

Aidha alisema pia mkakati wa kiendeleza wajasiriamali na vijana ni njia muafaka ya kuchochea maendeleo ya wananchi wa nchi za SADC.

Alisema anamaliza muda wake akiwa ameacha mikakati mizuri ya kufikia maendeleo ya viwanda na uchumi wa kati hivyo ni imani yake uongozi mpya utakuwa na mwanzo mzuri.

Ndaitwah alisema mwaka mmoja wa Uenyekiti wake umekuwa wa mafanikio kwa kupata ushirikiano wa nchi zote hivyo kuwaomba wajumbe wenzake waendeleze ushirikiano kwa mwenyekiti mpya.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa SADC, Dk. Stergomena Tax alisisitiza ili jumuiya iweze kuwa na tija ni lazima vijana washirikishwe kwenye maamuzi kwa kuwa ni nguzo muhimu ya uchumi na maendeleo.

"Ili tuende kwa pamoja ni lazima makundi yote yashiriki kwenye maamuzi muhimu ya jumuiya yetu kupitia majukwaa yao," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages