Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akimkabidhi zawadi ya picha
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Bi. Anne Kabagambe, baada
ya mkutano kati yao uliofanyika Jijini
Dar es Salaam ambapo Benki hiyo imeahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ya
Tanzania kwa kufadhili miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akisisitiza jambo wakati alipokutana
na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika
Bi. Anne Kabagambe, aliye katika ziara ya kikazi hapa nchini, Jijini Dar es
Salaam.
Na
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Uhusiano
wa Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania umeimarika baada ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia nchi 22 zilizoko Kanda ya Afrika, Bi. Anne
Kabagambe, kumhakikishia Waziri wa Fedha na Mipango kuwa Benki hiyo iko tayari
kutoa kwa Tanzania fedha zote za mkopo wa masharti nafuu kiasi cha dola za
marekani bilioni 1.7 zilizobaki katika mgao wa 18 wa IDA.
Bi.
Kabagambe ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi amesema hayo wakati wa mazungumzo
kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, yaliyofanyika
Jijini Dar es Salaam.
Alisema
kuwa kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kutolewa kabla ya kuanza mgao mpya wa 19
wa IDA utakaoanza Julai 2020, baada ya kukamilisha taratibu zote za upatikanaji
wa fedha hizo.
”Fedha
hizi zitaelekezwa katika kutekeleza miradi kadhaa muhimu ikiwemo ya Elimu, Afya,
Mradi wa kusaidia Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF, Awamu
ya Pili na Uendelezaji wa Miji na Masuala ya Uchumi Jumuishi Visiwani Zanzibar”
alisema Bi. Kabagambe
Aidha,
alipongeza hatua kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt.
John Pombe Magufuli, katika kupiga vita rushwa na ufisadi nchini pamoja na
kutekeleza miradi ya jamii kwa umahili mkubwa ikiwemo miradi ya kimkakati ya
reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa pamoja na mradi wa kufua umeme wa
maporomoko ya maji katika mto Rufiji wa Julius Nyerere.
Kwa
upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameiomba Benki hiyo
kuisaidia Serikali kwa kuipatia fedha za kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo
ya umeme, reli, maji safi na salama, kuimarisha sekta ya kilimo, viwanda, bandari,
rasilimali watu na masuala ya teknolojia ya habari na Mawasiliano-TEHAMA.
Alibainisha
kuwa miradi hiyo itachochea zaidi ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa
wananchi kwa kuwa nishati ya umeme itachochea ukuaji wa sekta ya viwanda hivyo
na kukuza ajira, wakati reli imara na ya kisasa itaimarisha mtandao wa reli na kuwa
uti wa mgongo wa maendeleo ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Afrika kwa ujumla.
Amepongeza
pia uamuzi wa Benki hiyo wa kuruhusu upatikanaji wa fedha kiasi cha dola za
Marekani bilioni 1.7 na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi
iliyokusudiwa katika sekta ya elimu, kusaidia kaya maskini kupitia TASAF,
kuendeleza masuala ya uchumi jumuishi Visiwani Zanzibar, masuala ya ardhi na
miundombinu ya barabara ili kuboresha shughuli za kiuchumi katika jamii.
Akitoa majumuisho ya mkutano wa Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango na Mgeni wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban, alisema kuwa Serikali inapongeza uamuzi wa
Benki wa kuendelea kuipatia fedha serikali ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi.
Mpaka sasa, Benki ya Dunia imefadhili miradi 28 ya
Maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.0 sawa na
takriban sh. trilioni 11.5, ambapo miradi 20 ni ya kitaifa yenye thamani ya
dola 4.065 bilioni na miradi 8 ni ya kikanda yenye jumla ya dola za Marekani
938 milioni.
No comments:
Post a Comment