UMOJA
wa Mataifa (UN) umeipongeza Serikali ya Tanzania kwa namna inavyotumia
vizuri rasilimali zake za ndani na hivyo kuiwezesha kutekeleza shughuli
mbalimbali za kimaendeleo sambamba na kupunguza utegemezi kutoka nje.
Pongezi hizo zimetolewa leo (Jumatano, Agosti 21, 2019) na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Bw. Alvaro Rodriguez
alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Mratibu
huyo Mkazi wa Umoja wa Mataifa ambaye alikwenda kumuaga Waziri Mkuu,
amesema kuwa Tanzania imeendelea kutumia vizuri mapato yake ya ndani kwa
kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii kama ujenzi wa hospitali na
vituo vya afya.
“Katika
kipindi changu cha miaka mitano ambacho nimefanya kazi Tanzania,
nimeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yanayofanywa na Serikali,
ikiwemo kuimarika kwa mahusiano kati ya Serikali na Umoja wa Mataifa na
taasisi zake nchini.”
Katika hatua nyingine,
Bw. Rodriguez ameisifu Serikali ya Tanzania kwa namna ilivyoweza
kuandaa na kuendesha vizuri mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Agosti 17
na 18 mwaka huu.
Mbali
na kuisifu Serikali pia kiongozi huyo amevipongeza vyombo vya habari
kwa jinsi vilivyoshirikiana na Serikali kuripoti matukio mbalimbali ya
mkutano huo. “Nawapongeza na wananchi kwa ushirikiano walioutoa kwa
Serikali wakati wote wa mkutano wa SADC.”
Kwa upande wake,
Waziri Mkuu amemshukuru kiongozi kwa pongezi alizozitoa ambazo ni
ishara kwamba anatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika kutumia vizuri
rasimali zake.
Waziri
Mkuu amesema “maelezo yaliyotolewa na Bw. Rodriguez yanaakisi kauli za
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba Tanzania si nchi
masikini na inayo uwezo wa kutoa misaada kutokana na rasilimali nyingi
ilizonazo. Watanzania waendelee kuiunga mkono Serikali yao.”
Pia,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza kiongozi huyo kwani alikuwa
kiungo kizuri kabaina ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa. Pia
atakumbukwa sana kutokana na mambo mengi aliyoyafanya kipindi cha
utumishi wake nchini Tanzania.
Awali,
Waziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini,
Mheshimiwa Balozi Thamasanqa Dennis Mseleku ambaye alikwenda kwa ajili
ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi nchini Tanzania.
Waziri
Mkuu alimpongeza Balozi huyo kwa ushirikiano na mchango alioutoa kwa
Serikali ya Tanzania katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo zikiwemo
za kiuchumi, elimu, afya, maendeleo ya jamii pamoja na kuimarisha
uhusiano baina ya nchini mbili hizo.
Kwa upande wake,
Mheshimiwa Balozi Mseleku ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa
ushirikiano mkubwa uliompatia katika kipindi chake cha utumishi akiwa
nchini na kwamba alitamani aendelee kubaki Tanzania.
No comments:
Post a Comment