NA SULEIMAN MSUYA
NCHI ya Tanzania ambayo
ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
imetaja mambo matatu muhimu ambayo itayapa kipaumbele katika kipindi cha mwaka
mmoja wa uongozi wake ndani ya jumuiya hiyo.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba
Kabudi wakati anazungumza na waandishi wa habari leo Agosti 21, 2019 jijini Dar
es Salaam.
Waziri Kabudi alisema pamoja
na mambo mengine wamejipanga kuelekeza mambo muhimu matatu yatakayopewa
kipaumbele kwa maslahi ya jumuiya.
Alisema jambo la kwanza
ni kuhakikisha lugha ya Kiswahili inazungumzwa kwenye nchi za jumuiya hiyo na
hiyo ni baada ya wakuu wa nchi hizo kuipitisha rasmi kuwa lugha ya nne.
Profesa Kabudi alisema
haikuwa kazi rahisi kukipigania Kiswahili kuwa lugha rasmi kwenye nchi hizo na
kwamba mkakati wake ulianza Machi mwaka huu na kuwataka Watanzania wajipange
vizuri kutumia fursa hiyo.
"Mkakati wa
kukipigania Kiswahili baada ya majadiliano ya muda mrefu kwenye kikao cha
mawaziri wa nchi wanachama wa SADC ,hatimaye Mwenyekiti wa Jumuiya alitoa ombi
kwa wakuu wa nchi na hatimaye imepitishwa.
"Ni jukumu letu
Watanzania kuhakikisha tunachangamkia fursa hiyo ikiwemo ya kufundisha
Kiswahili.Kwa sasa nchi za Kenya na Congo wananufaika sana na lugha hii maana
wengi wao wamekuwa walimu wa Kiswahili kwenye mataifa mengine.Nasi tuna kila sababu
ya kutumia fursa hii,"alisema.
Waziri Kabudi alisema
pamoja na fursa hiyo ya lugha ya Kiswahili kukubalika kutumika katika nchi 16
za SADC pia Watanzania wanapaswa kujifunza lugha nyingine kama Kifaransa na
Kireno.
“Ni faraja ambayo haina
kifani kwa Kiswahili kukubalika katika ukanda wetu naomba tutumie fursa hii
isijekuchukuliwa na watu wengine kwani kwa sasa walimu wengi wa Kiswahili
wanatoka Kenya na DRC Congo,”alisema.
Waziri Kabudi alisema
jambo la pili ambalo litapewa umuhimu ni kuhakikisha mkakati wa viwanda kwa
nchi wanachama unatekelezwa kama ambavyo wamekubaliana wakuu wa nchi hizo.
Alisema ambacho
kitafanyika ni kuwepo kwa mpango mkakati kwa kila nchi kufanikisha uwepo wa
viwanda kwa maendeo ya nchi hizo.
Aidha, alifafanua matarajio
yao ni kuona kunakuwa na kiwanda au viwanda vya mfano kwa nchi za SADC huku
akifafanua namna ambavyo Serikali ya Tanzania imejipanga kikamilifu kwenye eneo
hilo.
"Tanzania tumepiga
hatua sana katika viwanda , na hata kwenye maonesho ya bidhaa kwa nchi za SADC
bidhaa zetu zimekuwa kivutio kutokana na ubora wa bidhaa zetu.Waliotembelea
viwanda vyetu wamethibitisha na kufurahishwa na teknolojia ya hali ya juu
katika utengenezaji bidhaa,"amesema.
Alisema katika
kuhakikisha sekta hiyo inakuwa kwa kasi SADC imedhamiria kuondoa vikwazo vya
kisera na sheria, kusisitiza ubora wa bidhaa na kuondoa mizani nyingi ili
mizigo ifike kwa haraka.
Profesa Kabudi alitaja
jambo la tatu kuwa ni kuhakikisha nchi za jumuiya hiyo zinasimama kidete katika
kushinikiza jumuiya ya kimataifa kuoindole vikwazo nchi ya Zambabwe.
Alisema na katika
kutekeleza hilo wamekubaliana nchi zote za SADC Oktoba 25,2019 iwe ni siku
ambayo kutakuwa na shughuli au mijadala kwa kila nchi inayozungumzia Zimbabwe
kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.
Waziri Kabudi alisema
hakuna sababu ya nchi hiyo kuendelea kuwa na kuwekewa vikwazo wakati wananchi
wamefanya uchaguzi na kupata Rais wao
kwa uhuru na kusisitiza kuendelea kuiwekea vikwazo nchi hiyo ni kuendelea
kuwatesa wananchi.
"Kama kuliwa na
sababu za nchi hiyo kuwekewa vikwazo kwa sasa tunaamini havipo tena.Jumuiya ya
Kimataifa itoe vikwazo kwa Zimbabwe.Tumekubaliana katika mkutano wa Umoja wa
Mataifa mwaka huu tutakwenda na ajenda hii, lazima Zimbabwe iondolewe vikwazo
na kuwa Tanzania ndio Mwenyekiti wa SADC tumedhamiria katika hili,"amesema
Waziri Kabudi.
Kwa upande mwingine
Kabudi alisema Tanzania inaunga mkono ombi la nchi ya Burundi kujiunga SADC na
kwamba hadi sasa nchi hiyo imetimiza asilimia 70 ya vigezo vinavyohitajika.
Alisema Burundi
imebakiza vigezo viwili ambapo kimoja wapo ni kukubali kutoa ada ya kila mwaka
hivyo ikitimiza jumuiya hiyo itaangalia hatua nyingine.
Aidha, Prof. Kabudi
amevishukuru vyombo vya habari na waandishi kwa kuonesha uzalendo wa hali ya
juu kwenye kuripoti habari za SADC na kuwataka waendelea na utamaduni huo.
No comments:
Post a Comment