HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 24, 2019

VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WAONYWA

NA LYDIA LUGAKILA, KAGERA

 Katika kuelekea Uchaguzi wa Serikali za  Mitaa viongozi wa vyama vya siasa mkoani Kagera wameonywa kutowarubuni wananchi  kwa jambo lolote kwani ni kosa kisheria na haki hainunuliwi hivyo atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.
Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba mkoani  Kagera, Limbe Benard Limbe (pichani),  wakati akitoa ufafanuzi juu ya taratibu katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Bwana Limbe amesema kuwa haki ya kuongozwa, haki ya kuchagua na ya kuchaguliwa ni haki ambayo iko huru kwa sababu katiba ya nchi inaruhusu mtu achague ama achaguliwe hivyo ametoa onyo kwa wanasiasa kutothubutu  kufanya  mchezo  wa aina yoyote unaolenga  kuwarubuni wananchi kwani  sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa wananchi wanapaswa kutochagua kiongozi kwa  sababu ya kupewa kitu au msukumu  Fulani bali wachague kiongozi atakayewafaa.

Mkurugenzi huyo  amempongeza waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa kwa jinsi ambavyo amewashirikisha wadau mbali mbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa huku akiwataka wananchi kuondoa wasiwasi kwani serikali imejipanga ili kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa bora.

Amesema wananchi wajiandae kufanya uchaguzi wa amani ambapo taratibu na miongozi yote itatolewa na serikali na kuwa itakapowafikia wataiwasilisha katika vitongoji, mitaa na  kata na kila mhusika atapata taarifa inayostahili ili zoezi hilo liende katika hali inayotakiwa.
Katika hatua nyingine mkurugenzi  huyo amesema kuwa suala la uchaguzi litahusu Mtanzania halisi  yaani Raia awe wa kuzaliwa.

 ‘’Atakayehusika katika zoezi hilo ni Yule aliyeandikishwa na akapewa Utanzania  sio kwamba mtu amekuja kufanya kazi na anataka kupiga kura jambo hilo halitakubaliki alisema’’

Bwana limbe amesema kuwa wananchi wasiwe na hofu yoyote kwani Matangazo yatapita kila mahali na kuwa hadi muda huu tayari zoezi la kubainisha wale wote watakaoshughulika na zoezi zima la kuandikisha liko tayari.

Ameongeza kuwa  mtu atajitokeza kumrubuni  mwananchi ni kosa kisheria kwa sababu kufanya hivyo itakuwa ni kunyima mwananchi haki yake ya msingi ya kuweza kumchagua kiongozi aliye bora kiongozi ambaye ataweza kumletea maendeleo yake mwenyewe katika kutatua shida zake mbali mbali.

Amesema kuwa uchaguzi wa serikali za  mitaa ni uchaguzi mama kwa kuwa shughuli zote zinafanyika katika serikali za mitaa na wale viongozi ndio viongozi  wa ngazi ya mwanzo ambao  wananchi wanaishi nao na ambao wananchi ni rahisi kuwafikia.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kujiandaa kuchagua kiongozi aliye bora, kiongozi ambaye anaweza kuyaona matatizo ya wananchi kiongozi ambaye yuko tayari kuyatetea, kuyaona matatizo kwa kufuata sheria taratibu na kanuni. 

Hata hivyo amesema kuwa Miongozo na taratibu ya katiba imewapa muda mwingine tena wa kubainisha kiongozi wanayemtaka na ambaye ni bora ambaye ataweza kutatua mahitaji yao.

No comments:

Post a Comment

Pages