Na
Mwandishi Wetu, Dar
es Salaam
WAFANYAKAZI 51
waliopunguzwa kazi na Kampuni ya New Habari 2006 Ltd wameshindwa kufikia
muafaka na mwajiri wao katika Tume ya Usuluhishi wa Migogoro Kazini (CMA) Kanda
ya Dar es Salaam.
Kampuni hiyo ambayo Ofisa
Mtendaji Mkuu wake ni Mbunge wa Nzega Mjini na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein
Bashe, ilipunguza wafanyakazi zaidi ya 100, Mei 31 mwaka huu katika kile
kilichoelezwa kuwa ni kushindwa kujiendesha.
Shauri hilo Namba
CMA/DAR ES SALAAM/KIN/504/2019 la Juni 28 mwaka huu lililokuwa likisikilizwa
chini ya Msuluhishi wa Tume hiyo, Peter Mahindi, wafanyakazi wanamdai mwajiri
wao, jumla ya Sh bilioni 2 ambazo zimetokana na madai ya malimbikizo ya
mishahara na fidia kwa kuwaondoa kazini bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Kampuni hiyo imeshindwa
kueleza bayana kusudio la kuwalipa wafanyakazi hao stahiki zao kwa mujibu wa
sheria za kazi.
Katika shauri hilo
ambalo New Habari iliwakilishwa na Wakili, Neema Uisso kwa Tume hiyo alisema
hawezi kuwalipa wafanyakazi hao mafao yao kama wanavyotaka.
“Sina offer yoyote
niliyokuja nayo kutoka kwa mteja wangu”alisema
Wakili Neema mbele ya Msuluhishi wa CMA, Peter Mahindi.
Akizungumza katika
Ofisi za CMA Dar es Salaam muda mfupi baada ya shauri hilo kumalizika mwishoni
mwa wiki, Mwakilishi wa wafanyakazi hao, Khamis Mkotya alisema msingi wa kesi
hiyo ni kutokana na mwajili kuwapunguza kazini bila kufuata utaratibu pamoja na
kuwalipa stahili zao ikiwamo malimbikizo ya mishahara ya zaidi ya miezi mitano.
“Sheria za kazi zinataka pande zote mbili, yaani
mwajiri na mwajiriwa kutimiza wajibu wake, lakini sisi wafanyakazi wa NHL tumeitumikia
kampuni hiyo kwa muda mrefu lakini tumeondolewa kazini bila kulipwa malimbikizo
ya mishahara pamoja na stahili zingine tangu Januari hadi Mei mwaka huu.
“Katika vikao vya
majadiliano vya kupunguza wafanyakazi walitueleza kwamba tungelipwa stahiki
zetu zote hadi kufikia tarehe 15 Juni mwaka huu, lakini hadi muda huo ulipofika
walishindwa kutekeleza ahadi yao.
“Baada ya hapo tuliwapelekea
notisi ya siku saba kupitia kwa mwanasheria wetu ili jambo hili tulimalize
mezani jambo ambalo hawakutaka kulifanya”alisema Mkotya.
Akifafanua zaidi Mkotya
alisema kwa mara ya kwanza shauri hilo lilipangwa kusikilizwa CMA Julai 22 mwaka
huu ambapo Wakili wa mwajiri Neema ambaye awali alijitambulisha kwa wafanyakazi
kwamba ni mwanasheria kutoka Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye
Ulemavu aliieleza Tume hiyo kuwa mteja wake (New Habari) yupo tayari kulipa
stahiki nyingine bila fidia jambo ambalo lilipingwa na wafanyakazi hao kwa
maelezo kuwa fidia haiepukiki kulingana na mazingira ya namna walivyoondolewa kazini.
Kutokana na hali hiyo
Neema aliomba muda ili akashauriane na mteja wake kuhusu kipengele cha fidia.
Mkotya alisema
usuluhishi huo uliendelea Agosti 16 mwaka huu kwa pande zote mbili ambapo msuluhishi
alimtaka wakili wa New Habari kueleza hatua waliyofikia, ndipo Neema aliieleza
Tume hiyo kwamba hakuja na ‘offer’ yoyote kutoka kwa mwajiri.
Kutokana na maelezo hayo,
Mahindi alisema hatua ya kwanza ya usuluhishi wa shauri hilo imeshindikana na kuwauliza
wafanyakazi endapo wataendelea mbele au la.
“Kutokana na hali
hiyo, tumeamua kusonga mbele katika hatua ya pili ya Arbitration baada ya hii
ya kwanza kushindikana.”alisema Mkotya.
Madai
hayo ni pamoja na wakitaka mwajiri kuwalipa stahiki zao ikiwa ni pamoja na
malimbikizo ya mishahara ya zaidi ya miezi mitano,
kiinua mgongo pamoja na fidia kutokana na kupunguzwa kazi kinyume cha sheria na
taratibu za kazi.
No comments:
Post a Comment