Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akiangaalia katani iliyoanikwa, wakati
alipotembelea shamba hilo lililopo wilayani Kilosa. Kushoto anayetoa maelekezo
ni Meneja wa Rasilimali watu na Fedha Bw. Athumani Migeto. Kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Kilosa Mhe. Adam Mgoyi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
Wawekezaji wameshauriwa kufuata
taratibu, kanuni na sheria za kazi zilizopo nchini ili kuongeza ufanisi na tija
katika sekta ya kazi.
Hayo ameyasema na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea Shamba la Katani la China State
Farms lililopo wilayani Kilosa ikiwa ni ziara yake ya kutembelea maeneo ya
kazi.
Akizungumza mara baada ya
kuwasili katika shamba hilo alieleza
kuwa wawekezaji wakiwa kama waajiri lazima wahakikishe wanafuata sheria za kazi
katika maeneo yao ya uzalishaji kwa kuzingatia masuala ya msingi ya wafanyakazi
ili waweze kuzalisha kwa tija na kuwahamasisha kufanya kazi zao kwa juhudi.
“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea kuboresha mazingira ya
biashara ambayo yamekua yakivutia zaidi wawekezaji, hivyo sera nzuri zilizopo
nchini zimekuwa chachu kwa wawekezaji kuwekeza katika nchi yetu,” alisema
Mhagama
Alieleza pia, endapo
wawekezaji watafuata miongozo ya kisheria katika masuala ya kazi na ajira yatawarahisishia
utendaji wao wa kazi.
Akitolea mfano kuhusu
masuala ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi, likizo ya uzazi kwa wanawake, uwazi
wa mikataba ya ajira, uhuru wa mfanyakazi kujiunga na chama cha wafanyakazi,
haki ya kupatiwa vitendea kazi na maslahi ya wafanyakazi ni baadhi ya vitu vya
msingi ambavyo mwekezaji inabidi atoe kwa mfanyakazi wake kwa kuzingatia
taratibu na sheria.
Hata hivyo aliongezea kuwa ushirikiano
na vyama vya wafanyakazi ni jambo la muhimu kwa kuwa vimekuwa vikitetea masuala
ya wafanyakazi ambayo yamekuwa yakijitokeza katika maeneo yao ya kazi, pamoja
na kuwa na mkataba wa hali bora za wafanyakazi baina ya mwajiri na mwajiriwa.
Sambamba na hilo Mheshimiwa
Mhagama alitoa maagizo kwa timu ya wataalamu ambao aliambatana nayo kutoka Idara
ya Kazi, Wakala wa Usalama na Afya mahala pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Taifa wa
Hifadhi ya jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Tume ya
Usuluhisi na Uamuzi pamoja na Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi kuendelea kutoa
elimu kwa umma hususan wafanyakazi ili watambue sheria za kazi na namna taasisi
hizo zinaweza kuwasaidia katika kupata ufumbuzi wa masuala yao ya kazi.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa pongezi vilevile
kwa wawekezaji wa Shamba la Katani la China State Farms kwa kuwajali
wafanyakazi wao ikiwa na kuwajengea nyumba bora za kuishi wafanyakazi wao.
“Nimpongeze mwekezaji kwa
kuona umuhimu wa kuwajengea makazi wafanyakazi ambayo yatamaliza kabisa tatizo
la upatikanaji wa nyumba na umbali ambao wafanyakazi wamekua wakitumia kwenda
kazini,” alisema Mhagama
Pia, alitumi muda huo kuwahamasisha
wafanyakazi kutumia muda wao wa ziada katika mashamba yao binafsi na kujiunga
kwenye mashamba ya ushirika yatakayo wawezesha kupata soko la uhakika kutoka
kwa mwekezaji huyo ili waweze kuimarika kiuchumi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya
Kilosa Mhe. Adam Mgoyi alisema kuwa Sheria za kazi zimekuwa zikitoa mwongozo
mzuri kwa wawekezaji katika kuimarisha shughuli zao za uzalishaji, kutoa ajira
pamoja na kuchangia kwenye mapato ya nchi.
Kwa upande wake, Meneja wa
Kiwanda hicho Bw. Majuto Chitema alitoa pongezi zake kwa Mhe. Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kusifu juhudi alizonazo katika kuboresha na
kuwajengea mazingira wezeshi wawekezaji, kwani serikali yake imeweza mstari wa
mbele kuweka sera, miongozo, kanuni na sheria ambazo zimekuwa haziwabani
wawekezaji.
Miongoni mwa Wafanyakazi wa
China Estate Farms Bw. Azory Andrea alisema kuwa Serikali iendelee kuangalia
namna ya kuwa kuwasimamia wawekezaji waliopo nchini ili waweze kutekeleza
wajibu wao kwa wafanyakazi kwa mujibu wa sheria za kazi.
Kabla ya ziara hiyo Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama aliwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro kwa ajili ya kupata taarifa ya maeneo aliyoandaliwa kutembelea katika
ziara yake mkoani hapo.
No comments:
Post a Comment