*Awataka waache kugombana, watekeleze majuku yao ipasavyo
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya
Shinyanga, Bw. Geoffrey Mwangulumbi pamoja na Mwekahazina wa Manispaa
hiyo, Bw. Pascal Makoye kuwa anawataka wabadilike na waache kugombana na
badala yake watekeleze majukumu yao ipasavyo.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bibi Zainab Telack
azisimamishe kazi kampuni zote zilizopewa zabuni ya kukusanya mapato
katika Manispaa hiyo kwa kuwa zimeshindwa kufanya kazi vizuri na zina
madeni.
Waziri
Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Agosti 9, 2019) wakati
alipozindua nyumba 10 za Askari Polisi katika Manispaa ya Shinyanga eneo
la Kambarage. Mradi huo umetokana na fedha kiasi cha sh. milioni 225
zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli.
Amesema
viongozi hao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia
kikamilifu zoezi la ukusanyaji wa mapato na kutoa kazi hiyo kwa kampuni
zisizokuwa na uwezo. Amesema mwaka jana walikadiria kukusanya sh.
milioni 800 na badala yake walikusanya sh. milioni 500.
Waziri
Mkuu amesema Manispaa hiyo haiwezi kusonga mbele kimaendeleo iwapo
viongozi wake hawaelewani wanagombana kila siku. “Mkurugenzi na wenzako
nawaonya kwa mara ya mwisho badilikeni na hakikisheni mnatekeleza
majukumu yenu ipasavyo yakiwemo ya ukusanyaji wa mapato.”
Akizungumzia
kuhusu nyumba za Askari Polisi, Waziri Mkuu amesema lengo la ujenzi wa
nyumba hizo ni kuhakikisha askari wanaishi katika mazingira mazuri
yatakayowawezesha kutekeleza vizuri majukumu yao. “Ili waweze kutekeleza
vizuri majukumu yao lazima wawe na makazi mazuri”.
Pia,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa askari waliopewa funguo kwa ajili ya kuishi
katika nyumba hizo wahakikishe wanazitunza vizuri na hata inapotokea
wamehamishiwa kwenda katika vituo vingine, wale watakaohamia wakute
nyumba hizo zikiwa katika mazingira mazuri.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa nyumba hizo ni endelevu, ambapo
pia amezitaka idara mbalimbali za Serikali ziendelee na mchakato wa
ujenzi wa nyumba zake kwani wakiwa na nyumba nyingi itasaidia kupunguza
idadi kubwa ya askari wanaoishi uraiani.
Awali,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao alisema awali
fedha zilizotolewa zilikuwa zijenge nyumba tisa za vyumba viwili lakini
kutokana na ubunifu waliweza kuboresha mradi huo kwa kuongeza nyumba
moja sambamba na kuongeza chumba kimoja, hivyo kuufanya mradi huo kuwa
na nyumba 10 zenye vyumba vitatu vya kulala.
Pia
alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa upendo wake mkubwa kwa Jeshi la
Polisi Tanzania kwa kulipatia fedha za kuboresha makazi ya askari. Mradi
huo umekamilika kwa gharama ya sh. milioni 278, 565, 500 wastani wa
gharama za ujenzi kwa nyumba moja ni sh. milioni 27, 856, 550. Alisema
kiasi cha nyongeza cha sh. milioni 53, 565,500 zilitolewa na wadau
mbalimbali.
No comments:
Post a Comment