HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 03, 2019

TASAF waombwa kuongeza idadi ya walengwa

NA MWANDISHI WETU, SINGIDA

MKURUGENZI wa Manispaa ya Singida mkoani Singida, Bravo Lyapembile, amewaomba watendaji wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini zaidi (TASAF) awamu ya tatu kuwafikia wananchi wengi zaidi wilayani humo.

Lyapembile alisema hayo mjini hapa juzi alipotembelewa na baadhi ya maofisa wa TASAF waliokuwa wakikagua maendeleo na changamoto za utekelezaji wa sehemu ya kwanza kwa awamu ya tatu na namna ya kukabiliana nazo.

Akizungumzia changamoto alizozibaini kwenye mpango huo alisema kaya nyingi zenye sifa ya kuingizwa katika mpango wa TASAF zimeachwa huku akibainisha uwepo mkubwa wa kaya maskini katika manispaa hiyo. 

"Ni mpango mzuri wenye nia ya kuondoa umaskini kuanzia ngazi ya kaya ila nawashauri muongeze idadi ya walengwa wenu maana zipo kaya nyingi maskini zaidi yaani kipato chao ni chini ya Sh. 1,000 kwa siku hawajafikiwa na TASAF.

"Lakini pia nawashauri wanufaika wa mpango huu kufanya miradi endelevu na mikubwa kwa maana ya kama anafuga kuku afuge kwa wingi zaidi na muda mrefu.

"Mnafanyakazi nzuri sana kuisaidia serikali kukabiliana na umaskini na hayo ndio malengo ya Rais wetu John Magufuli... mnawezesha kipato kwa maana ya uhakika wa chakula, huduma za afya kama mlivyojenga zahanati ya Ugauga na elimu pia kwa kusisitiza watoto kwenda shule nawashukuru sana," alisema Lyapembile.

Kuhusu huduma za maofisa ugani alisema wanawafikia wananchi kwa wakati huku akisisitiza kwamba hajapokea malalamiko ya kukosekana kwa huduma hizo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Manispaa ya Singida inakusanya zaidi ya Sh. milioni 250 kwa mwezi sawa na zaidi ya Sh. bilioni tatu kwa mwaka na kubainisha kwamba wanaendelea kutoa mikopo nafuu kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu.

"Mwaka 2017/2018 tuliwakopesha Sh. milioni 180 na mwaka uliofuata 2018/2019 tumewakopesha Sh. milioni 136 changamoto yetu mikopo hairudi kwa wakati na mingine hairudi kabisa," alisema mkurugenzi huyo.

Juma Nzogo ni Mratibu wa TASAF Manispaa ya Singida, alisema mpango huo imefanikiwa kutekeleza baadhi ya miradi ya kijamii iliyosimamiwa na walengwa wa mpango huo.

Nzogo aliishukuru ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa kwa ushirikiano wanaowapa wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye jamii ya walengwa wa TASAF.

No comments:

Post a Comment

Pages