Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha akionesha moja ya chumba kilichojengwa maarufu kama Tegesha katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wakati akikagua kazi ya uthamini wa fidia inayofanywa na Ofisi yake katika eneo la Nyamongo kupanua mgodi wa Dhahabu wa North Mara ili kupisha ujenzi wa bwawa la maji taka juzi. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM NYAMONGO
Zoezi la uthamini
kulipa fidia kwa wananchi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara kupisha
upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu North Mara kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Maji
Taka limekumbwa na changamoto kufuatia baadhi ya wananchi kujenga nyumba ama
kuongeza sehemu za nyumba zao maarufu kama ‘Tegesha’ ili kujipatia faida
kupitia thamani ya fidia.
Wathamni katika zoezi
hilo walibaini tofauti kubwa katika uthamini walioufanya awali na pale
walipoenda kwa mara ya pili kwa ajili ya uhakiki ambapo ilibainika baadhi ya
vyumba katika nyumba zilizofanyiwa uthamini kuwa wazi baada ya waliokuwa
wakiishi kuondoka baada ya kuthaminiwa.
Imeelezwa kuwa lengo
wananchi wanaofanya ujanja wa ‘Tegesha’ ni kujipatia posho ya makazi ambayo kwa
kawaida hutolewa kama fidia kwa wamiliki kulingana na idadi ya vyumba kwenye
nyumba ya mmiliki.
Kwa mujibu wa Wathamini
wa zoezi hilo, mbali na wamiliki walioathirika na zoezi hilo kulipwa gharama
nyingine kama vile nyumba na mazao pia hulipwa posho ya makazi kwa kipindi cha miezi 36 lengo kumuwezesha
mpangaji kupata mahali pa kuishi kabla ya kuanza zoezi la kuondolewa.
Mwandishi wa Gazeti
hili alishuhudi moja ya nyumba iliyopo kitongoji cha Kigonga A katika kijiji
cha Matongo ikiwa na vyumba ishirini na moja wakati nyumba hiyo ilistahili kuwa
na vyumba vitatu na baadhi ya vyumba havina hata madirisha.
Mthamni Mkuu wa
Serikali Evaline Mugasha ambaye alitembelea baadhi ya nyumba hizo kukagua
maendeleo ya kazi ya uthamini katika eneo hilo aliweka wazi kuwa Ofisi yake
inafanya kazi kwa kufuata sheria ya Uthamini na hatua kali zitachukuliwa kwa
mtu atakayeonekana kufanya udanganyifu kwa kwa lengo la kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa Mugasha,
zoezi la uthamini katika eneo la Nyamongo linalohusisha vitongoji vitatu katika
kijiji cha Matongo limekuwa likifanyika kwa uwazi na kushirikisha pande zote
wakati wa kuorodhesha mali na kufafanua kuwa hata mwananchi asiyeridhika na
uthamini katika eneo lake hupewa fomu maalum ya kujaza lengo likiwa
kutoa haki.
‘’Tumeona watu walihamisha magodoro, vitanda
na mizigo mingine lengo ni kupata posho ya makazi ili kujipatia faida na cha
kushangaza baadhi ya wapangaji hawajui hata choo cha nyumba wanayoishi kilipo,
ofisi yangu haitavumilia vitendo hivyo kila mtu atalipwa anachostahili’’
alisema Mugasha.
Mthamini kutoka Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Lazaro Magumba alieleza kuwa wakati zoezi la uthamini
kumekuwa na changamoto hasa wakati wa kukagua mali za wananchi kutokana na
baadhi yao kuwa na dhana ya kujipatia utajiri kupitia mradi huo ambapo hufanya
maendelezo ya kuegesha maarufu kama ‘tegesha’ ili kulipwa fedha nyingi.
‘’ Wananchi wanajenga
nyumba zilizopangana na hakuna hata nafasi na wakati wa uthamni usiku kucha
watu wanahamisha vyombo, magodoro na wengine hata wanyama ili ionekane ni
makazi halali’’ alisema Lazaro.
Alisema wanachokifanya
wao ni kukagua kwa awamu kwa lengo la kujiridhisha kama kweli walionekana
wakati wa uthamini kama ni wakazi halali ama walienda kutegesha.
Baadhi ya wakazi wa
kijiji cha Matongo wilayani Tarime mkoa wa Mara ambao hawakupenda majina yao
yawekwe wazi kutokana na sababu za kiusalama walikiri kuwepo mchezo huo wa
Tegesha lakini walidai hufanywa na watu wasio wakazi wa muda mrefu katika
kijiji hicho bali walienda kwa lengo la kujipatia faida kupitia zoezi hilo.
Kwa mujibu wa wakazi hao, baadhi ya wananchi kutoka nje ya kijiji hicho walinunua
nyumba ama maeneo kwa wenyeji na kuongeza vyumba na kuwakodisha watu kuishi ili
kuvizia zoezi la uthamini wa fidia wapate faida.
Kwa muda mrefu wananchi
wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa mara hasa wale wanaoishi vitongoji
vinavozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wamekuwa wakilalamikia uchafuzi wa
mazingira hasa maji yanayovuja kutoka Mgodi huo kuwa yana sumu inayoathiri afya
zao jambo lililomlazimu Rais John Pombe Magufuli wakati wa ziara yake katika
eneo hilo kuagiza kufanyika utafiti ili kubaini ukweli huo.
No comments:
Post a Comment