Geofrey Kazaula na Bebi Kapenya - Kigoma
Wananchi
katika Halmashauri
ya Wilaya ya Kigoma wanatarajia kunufaika na Ujenzi wa Madaraja ya mawe
unaofadhiliwa na
Serikali ya Ubelgiji chini ya mradi wa Kilimo endelevu katika Mkoa wa
Kigoma (Sakirp – Enabel) na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini TARURA.
Akizungumza na waandishi wa
habari wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Kigoma Bi. Pendo E. Mangali ameeleza kuwa mradi huo uliibuliwa na wananchi
baada ya kueleza changamoto wanayokutana nayo katika kusafirisha mazao yao
kutoka mashambani hadi majumbani na kwenye masoko.
Kiongozi huyo amebainisha
kuwa mradi huo wa Ujenzi wa madaraja ya mawe unalenga kutatua kero ya usafiri
na usafirishaji wa mazao na kwamba wananchi walihamasishwa na wakakubali
kujitokeza katika kusomba mawe na kushiriki kujenga madaraja hayo.
“Nitumie
fursa hii kuwapongeza sana wananchi wa Halmashauri ya Kigoma kwani wanafanya
kazi sana, baada ya kugundua kuwa wanashindwa kusafirisha mazao yao kutoka
mashambani hadi sokoni kwa pamoja tuliamua kuanza ujenzi wa madaraja ya mawe”, amesema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo amebainisha
kuwa baada ya kukamilika kwa madaraja hayo kazi itakayokuwa imebaki ni Kufungua
barabara za kuunganisha mashamba na hatimaye kuwezesha wananchi kufikisha mazao
yao sokoni kwa urahisi na kukuza kipato chao.
Kwa upande wake Meneja wa
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kigoma Mhandisi Pharles E. Ngeleja ameeleza kuwa Ujenzi wa madaraja kwa teknolojia ya kutumia
mawe ni wa gharama nafuu na kwamba una
washirikisha wananchi moja kwa moja kwa kukusanya vifaa vinavyopatikana katika
mazingira yao hususani mawe na wafadhili wanatoa vifaa vya viwandani
visivyopatikana kwenye mazingira mfano simenti huku TARURA wakisimamia shughuli
za ujenzi .
Akiongea kwa
niaba ya wananchi wanaoshiriki katika ujenzi wa madaraja hayo, Mwenyekiti wa
Kijiji cha Nyabigufa Ndg. Johnphace
Kabora Tunzwe amesema kuwa changamoto ya
usafiri ni kubwa hasa kipindi cha masika na hivyo tayari wameamua kujitolea kwa
kukusanya mawe ili kujenga madaraja .
“Kwanza nawashukuru
TARURA, Sakirp Enabel na Halmashauri ya Kigoma kwani mwanzo tulidhani kuwa kazi
hii ni ngumu sana na haiwezekani lakini sasa kama mnavyoona tayari tumeanza
kukamilisha ujenzi wa daraja” amesema Kiongozi huyo.
Aidha ameongeza
kuwa baada ya kukamilisha ujenzi wa daraja, kazi itakayokuwa imebaki ni Kufungua
barabara za kufika mashambani ili kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao yao na
kwamba anaimani kuwa Serikali kupitia
TARURA watafungua barabara .
Naye Meneja
mshauri wa mradi huo chini ya Serikali ya Ubelgiji Ndg.
Steven Hollevoet ameeleza kuwa Teknolojia ya ujenzi wa madaraja ya mawe ni ya
muda mrefu hasa katika nchi za Ulaya na Asia na sasa wameileta Tanzania ili
kuwafundisha wananchi kujenga madaraja kwa gharama nafuu kwasababu vifaa
vinavyotakiwa kama mawe na mchanga vinapatikana kwa urahisi.
Hadi sasa madaraja sita
yamekamilika na madaraja tisa yapo katika hatua mbalimbali huku lengo likiwa ni
kukamilisha madaraja kumi na tano ifikapo mwezi Desemba, 2019.
No comments:
Post a Comment