HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 11, 2019

Tanzania, Misri kushirikiana kukuza uchumi, viwanda

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Biashara kati ya Tanzania na Misri jijini Dar es Salaam (Picha na Suleiman Msuya).

NA SULEIMAN MSUYA

SERIKALI ya Tanzania imesema inajipanga kutafsiri kwa vitendo ushirikiano wake na nchi ya Misri ili kuchochea ukuaji wa uchumi na viwanda.

Hayo yameswa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi wakati akifungua Wiki ya Biashara iliyoandaliwa na nchi ya Tanzania na Misri jijini Dar es Salaam.

Balozi Mwinyi alisema Tanzania na Misri zimekuwa na uhusiano wa miaka mingi ambao ulijikita katika siasa na jamii hivyo wakati umefika kubadilika na kujikita katika viwanda na biashara zaidi.

Alisema nchi ya Misri imeendelea kwa kiwango kikubwa katika sekta ya viwanda na biashara hivyo ni vema Tanzania ikatumia fursa ya maendeleo kuchochea ukuaji wa uchum na viwanda kama Rais John Magufuli na Serikali yake wanavyotamani.

"Kwa miaka mingi tumekuwa tukishirikiana na Misri kwa wao kununua rasilimali za Tanzania zikiwa katika hali ya malighafi hivyo tunapaswa kuondoka huko ili kunufaisha wakulima kwa kuzichakatai," alisema.

Alisema takwimu zinaonesha kila mwaka Misri imekuwa ikiingiza bidhaa nyingi nchini ambapo kwa mwaka jana iliingiza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 42 kutoka dola milioni 24 mwaka 2017.

Naibu Katibu Mkuu alisema matarajio ya Serikali ni kuona kunakuwepo na uwiano sawa wa uaguzaji na upelekaji wa malighafi ili kila  nchi iweze kunufaika.

Balozi Mwinyi alisema wakati wa kupeleka malighafi umepitwa na wakati hivyo wafanyabiashara na wazalishaji wa viwnada wanapaswa kufikiria upelekeaji bidhaa zilizochakatwa.

Kwa upande wake Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mohamed Abulwafa alisema Wiki hiyo ya Biashara imeshirikisha kampuni 14 kutoka nchini kwao na kwamba baadhi zitawekeza nchini hivi karibuni.

Abulwafa alisema kampuni hizo 14 zinajihusisha na vifaa tiba, dawa, vifaa vya ujenzi, nishati ya jua, kemikali na uhandisi wa viwanda.

"Sisi na Tanzania tuna ushirikiano wa siku nyingi hivyo kwa sasa tunataka kujikita kwenye uwekezaji wa viwanda vya aina mbalimbali ili kuchochea ukuaji wa uchumi," alisema.

Akizungumzia wiki hiyo Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Zachy Mbenna alisema itachangia ukuaji wa uchumi kwa kasi kati ya nchi hizo.

Alisema Misri ni moja ya nchi ambayo ina kampuni nyingi zilizowekeza nchini na kwamba matarajio yao ni kuona uwekezaji unaongezeka.

"Taarifa za mwaka jana zinaonesha Misri imewekeza zaidi dola milioni 900 kupitia kampuni zaidi ya 22 hivyo tukiongeza nguvu uwekezaji utaongezeka" alisema.

Mbenna alisema Misri inanua bidhaa za mazoa kama kawahawa, chai, tumbaku na kutoa huduma ya elimu kwa Watanzania.

Mkurugenzi huyo alisema ili kuweza kunufaika na ushirikiano huo ni lazima Watanzania kushirikiana na wawekezaji wa Misri kuwekeza.

Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara, Viwanda na Kilomo Tanzania (TCCIA), Paul Koyi alisema shirikisho hilo litautumia ushirikiano baina ya Tanzania na Misri katika kuleta matokeo chanya kwa haraka.

Koyi alisema fursa hiyo ikitumika vizuri ni wazi kuwa pande zote zitanufaika kiuchumi, maendeleo na kijamii.

No comments:

Post a Comment

Pages