Daktari wa mionzi ya nyuklia kutoka Hospitali ya Aga Khan Dk. Raghu, akimuhudumia mgonjwa katika mashine ya kisasa ya mionzi ya nyuklia yenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa magonjwa ya saratani, figo, moyo na ubongo. (Na Mpiga Picha Wetu).
NA JANETH JOVIN
JUMLA ya watu 835 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa katika
Hospitali ya Aga Khan kwa kutumia mashine ya kisasa ya mionzi ya nyuklia (Spect
Gamma Camera), ambao inauwezo wa kugundua mapema matatizo yanayowasumbua mtu na
kwa kiasi gani yameenea mwilini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Mkurugenzi wa Tiba na Mkuu wa Idara ya Ladiolojia wa hospitali hiyo, Dk.
Ahmed Jusabani amesema asilimia 99 ya wagonjwa yaliochunguzwa ni ya mifupa,
figo, moyo, mfumo wa mkojo pamoja na saratani zote ikiwamo ya matiti na shingo
ya kizazi.
Amesema uwepo wa mashine hiyo imeisaidia hospitali kuweza
kuwatambua wagonjwa wenye matatizo na kuwapatia huduma bora kwa haraka kabla ya
tatizo alijaenea mwilini.
Jusabani amesema hospitali hiyo ya Aga Khan kwa kushirikiana
na Kampuni ya Siemens imeweza kuwa hospitali ya kwanza binafsi Tanzania
kuwekeza katika kutoa huduma hiyo ya mionzi ya nyuklia hivyo kuwawezesha watanzania
kupata huduma bora hapa nchini pasipo kwenda nje ya nchi kufuata tiba.
“Mashine hii imekuwepo hospitali hapa kwa miaka mitano sasa
na imekuwa msaada kwa wagonjwa wengi ambao wameanza kuwa na dalili za saratani
na magonjwa mengine.
Teknolojia iliyopo kwenye mashine inauwezo wa kugundua
magonjwa mapema zaidi na kuona yameenea sehemu ya mwili kwa kiasi gani, pia
kugundua tiba anayopatiwa mgonjwa kama inafanya kazi au la,” amesema na
kuongeza.
“Nisisitize kuwa mashine hii haitumika kwa magonjwa ya kansa
tu bali inatumika kwa magonjwa mengine yasikuwa ya saratani, na inatumiwa na
watu wazima hata watoto wachanga pia wanaweza kufanyiwa kipimo kwa kutumia
mashine hii,” amesema.
Naye Daktari Bingwa wa Mionzi ya Nyuklia nchini, Dk. Tausi
Maftah amesema mionzi hiyo ya nyuklia inauwezo wa kutambua magonjwa katika hali
ya awali hivyo kumsaidia mgonjwa kufanya matibabu na kupona kabisa.
Hata hivyo amesema changamoto iliyopo ni uwepo wa idadi
kubwa ya watu wanaotaka kufanya vipimo vya saratani lakini wanashindwa kutokana
na uchache au kukosekana kabisa kwa mashine hizo katika hospitali zingine.
“Mpaka sasa mashine za mionzi nchi nzima zipo tatu tu,
yaani hapa Aga Khan, Ocean road na Bugando Mwanza, ukiangalia hii utaona jinsi
ambavyo bado tunahitaji kuwa na vifaa hivi katika hospitali nyingine ili
wananchi waweze kupima na kupata huduma,” amesema.
Kwa upande wake Mtaalamu wa mionzi kutoka Marekani
katika Chuo cha Albert Binsten, Dk. Tony
Abraham amesema ni muhimu mashine hiyo ikawepo nchini kwa wingi kwani inawasadia
madaktari kufanya uchunguzi kwa usahihi na kwa mgonjwa kupata matibabu kwa
haraka.
No comments:
Post a Comment