HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 05, 2019

Taasisi ya Usuluhishi yaomba mabadiriko ya sheria

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Juma
NA JANETH JOVIN
 
TAASISI ya Usuluhishi Tanzania imeiomba Mahakama ya Tanzania kusaidia katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Usuluhishi ya mwaka 1931 kwa kuwa sheria hiyo hivi sasa imepitwa na wakati.

Sheria ya Usuluhishi ya mwaka 1931 ilifanyiwa marekebissho mara moja tangu Tanzania ipate Uhuru wake ambapo marekebisho hayo yalifanyika mwaka 1971.

Maombi hayo yamewasilishwa jijini Dar es Salaam leo na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Gabriel Malata wakati ujumbe kutoka taasisi hiyo ulipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa. Ibrahim Juma ofisini kwake kwa lengo la kujenga mahusiano ya kiutendaji kati yake na Mahakama ya Tanzania na pia kutambulisha uongozi mpya wa Taasisi hiyo.

Akizungumzia mchakato wa mabadiliko ya Sheria hiyo ya Usuluhishi, Malata aliiomba Mahakama kuishirikisha taasisi hiyo kwa karibu katika mchakato wa mabadiliko ya sheria hiyo na hususan katika hatua ya utengenezaji wa kanuni.

Amesema Taasisi ya Usuluhishi Tanzania iko tayari kutoa maoni na mapendekezo pindi hatua hiyo itakapofikiwa na kuongeza kuwa hivi sasa taasisi hiyo imejikita katika kutoa elimu husika katika Shule ya Sheria (Law School of Tanzania) ambapo wanafanya vipindi ili waweze kupata wasuluhishi bora hapo baadaye.

Mwenyekiti huyo amesema taasisi yake inao mfumo unaowatambua Wasuluhishi hai na hivyo ameiomba Mahakama kuishirikisha ili wapatikane wasuluhishi hai.
Kwa Upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Juma amesema Mahakama iko tayari kurekebisha kanuni za usuluhishi pale inapobidi kufanya hivyo ili tasnia ya usuluhishi ifanye kazi vizuri na kuwasaidia wananchi kwa haraka.

Amesema suala la usuluhishi ni muhimu kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwa litasaidia kupunguza idadi ya kesi mahakamani.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, utafiti unaonyesha kuwa suala la usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama linaweza kufanyika katika ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama ya juu.

Aidha, Jaji Mkuu ameishauri taasisi  hiyo ya usuluhishi kuhakikisha inatoa zaidi elimu juu ya masuala ya usuluhishi kwa kuwa wananchi wengi bado hawana uelewa wa masuala hayo.

No comments:

Post a Comment

Pages