Sharifa Mussa Mkazi wa kitongoji cha Chanika
akimuonesha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi madai
yake ya fidia ya ardhi ambayo bado hayajalipwa wakati wa mkutano wa hadhara wa
utatuzi wa kero za ardhi kwa wakazi wa mji wa Handeni katika uwanja wa Soko la
Zamani Chanika maarufu Nyerere Square Wilayani
Handeni Mkoani Tanga.
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameziagiza Halmashauri za Miji pamoja na watu wenye
mashamba makubwa wahakikishe wanawalipa fidia Wananchi wote ambao hawajalipwa
kwa muda mrefu tangu kufanyika kwa tathmini kwani wananchi wengi wamekuwa
wakiishi ndani ya mashamba yao kwa muda mrefu na wakiamishwa hawalipwi fidia zao kwa
miaka mingi na wengine kuondolewa bila kulipwa kabisa.
Waziri Lukuvi meyasema hayo
alipofanya ziara Wilayani Handeni Mkoani Tanga wakati wa kusikiliza kero za
wananchi katika uwanja wa Soko la zamani Chanika maarufu Nyerere Squre Katika
mkutano huo Waziri wa Ardhi aliongozana na Mkuu wa Wilaya hiyo Godwin Gondwe
akiwa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Handeni Mhe. Omari Abdallah Kigoda na
watendaji mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Kupitia kampeni yake ya "FUNGUKA
KWA WAZIRI" Mhe. Lukuvi
amesikiliza kero za ardhi za wananchi zaidi ya 200 wa wilaya ya Handeni zilizowasilishwa
kwake. Kampeni hiyo iliyoanza saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni ambapo wakazi
wengi wa mji huo wamelalamikia suala la kulipwa fidia ndogo au kutokulipwa
fidia zao kabisa.
Mh. Lukuvi amesema Halmashauri
nyingi zimekuwa na pupa za kupanga viwanja bila kuwalipa wananchi fidia na hata
ikitokea wakalipa fidia basi fidia itakuwa ndogo sana kwani kwa kufanya hivyo
kutazidisha migogoro mingi ya ardhi isiyo ya lazima, hivyo amezitaka
halmashauri kupitia upya madai ya wananchi na kuwalipa stahiki zao.
”Kwa kuwa hapa sasa mashamba mengi
ya mji huu yamegeuka kuwa ni miji, lazima hawa watu muwafidie viwanja zaidi
kuliko pesa kama wanataka pesa basi wauze wenyewe hivyo viwanja, hamuwezi
kuwapa shilingi milioni tatu wakati nyinyi mnauza viwanja milioni kumi.
Kumekuwepo
na unyang’anyi na kuwalazimisha watu kupima viwanja kwa fidia kidogo. Na kwa
mujibu wa sheria ya fidia kama hujamlipa mwananchi kwa miaka zaidi ya miwili
basi inatakiwa ufanye tathmini upya”.
Hata hivyo Mh.Lukuvi ameshangazwa na
wingi wa migogoro ya Ardhi ambayo ilikwisha patiwa ufumbuzi wake na mingine
ilikwisha tolewa hukumu na Mahakama lakini cha kushangaza bado wananchi
wanacheleweshewa haki zao hivyo kuwaamuru Maafisa ardhi kuhakikisha
wanashughulikia swala hilo haraka iwezekanavyo kwani asingependa kuona swala
hilo likijirudia tena.
Mhe. Lukuvi amesema kuwa amebaini 90%
ya Wananchi wa Handeni hawana uwelewa juu ya hatimiliki ya ardhi zao
wanazomiliki kwani ameshangazwa sana kuona wengi wao hawafahamu mipaka ya
maeneo yao hali inayopelekea kuzuka kwa migogoro ya mipaka hivyo amewaasa
wananchi kuyafatilia maeneo yao na kuyapatia hati miliki ili kuyalinda na
wavamizi kwani Hati ndio kielelezo namba moja kinachotambulika kisheria.
"mimi kama Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi ipo migogoro ambayo nina uwezo wa kuitafutia
ufumbuzi kutokana na mamlaka niliyonayo na ndio maana nimeamua kuwa na kampeni
ya Funguka kwa Waziri ili kusikiliza kero mbalimbali za Ardhi lakini hii
migogoro ya mtu na mtu inatakiwa kutafutiwa ufumbuzi ndani ya ofisi zenu za
ardhi au wilaya" Amesema Waziri Lukuvi.
Hata hivyo baada ya kusikiliza kero
za wananchi Waziri Lukuvi ameahidi kuanzisha Baraza jipya la Ardhi na Nyumba la
Wilayani Handeni kwani wananchi wamekuwa wakisafiri hadi Wilayani Korogwe
kusikiliza mashauri yao jambo ambalo limekuwa na ucheleweshaji wa kusikiliza na
kutatua kero za ardhi kwa wakati kwani ndio chanzo cha migogoro mingi Wilayani
hapo.
Aidha, akifunguka mbele ya Waziri
Bi. Telessa Petro Gumbo ambae ni mkazi wa Handeni amelalamikia uvamizi wa uliofanywa
katika shamba lake ambapo amemuomba Waziri Lukuvi kuingilia kati swala lake la
kutolulipwa fidia baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kulimega eneo lake
na kupitisha barabara hali inayomlazimu kulipwa fidia ya eneo hilo.
Naye, Bi. Amina Ali Kiale ambae pia
ni mkazi wa Handeni amemlalamikia Waziri lukuvi kwa baadhi ya watendaji wa
Ardhi ambao sio waaminifu kushiriki katika vitendo vya kudhurumu ardhi kwa
kuwacheleweshea hati zao kwa muda mrefu wanapokuwa wanazifatilia.
Katika kutoa shukurani kwa Mhe.
Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe amemshukuru Mh. Lukuvi kwa
kitendo cha kuifanya programu hiyo ya FUNGUKA KWA WAZIRI katika Wilaya yake ya
Handeni kwani imeweza kutatua migogoro ya ardhi iliyodumu muda mrefu na kuahidi
kushughurikia migogoro iliyobaki katika ofisi yake ya Wilaya.
No comments:
Post a Comment