HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 05, 2019

WAZIRI MKUU AKAGUA MRADI WA MAJI MANYONI

*Unatarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 10

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa mradi wa maji wa Kintiku – Lusilile ulioko Manyoni ambao awamu yake ya kwanza inatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 22, mwaka huu.

Akizungumza na watumishi na wakadarasi leo (Ijumaa, Oktoba 4, 2019) mara baada ya kukagua mradi huo akiwa njiani kuelekea Manyoni, Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na ujenzi huo pamoja na kasi ya mkandarasi.

Waziri Mkuu ambaye ameanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Singida, alielezwa kwamba mradi huo utahudumia vijiji 11 vya Kintinku, Lusilile, Maweni, Mvumi, Ngaiti, Chikuyu, Mwiboo, Mbwasa, Mtiwe, Makutupora na Chilejeho ambavyo viko kando ya barabara kuu itokayo Singida kwenda Dodoma.

Akitoa taarifa ya mradi mbele ya Waziri Mkuu, Meneja wa RUWASA, Injinia Gabriel Ngongi alisema wananchi zaidi ya 55,000 watanufaika na mradi huo pindi utakapokamilika. Alisema awamu ya kwanza imegharimu sh. bilioni 2.46.

Akizungumzia halia halisi ya utekelezaji wa mradi huo, alisema ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji la lita 300,000 limekamilika lakini bado liko kwenye hatua ya umaliziaji. “Birika la kuhifadhia maji lemye ujazo wa lita milioni mbili limekamilika, bado shughuli za umaliziaji,” aliongeza.

Alisema ujenzi wa uzio, nyumba ya kuhifadhia mitambo na nyumba ya mlinzi umekamilika licha ya kuwa bado kuna kazi ndogo za umaliziaji.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Itigi.

No comments:

Post a Comment

Pages