HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 11, 2019

Benki ya Stanbic kuzindua mashine mpya za kupokea fedha, moja ya juhudi za kuchochea ukuaji wa sekta binafsi

Dar es Salaam, Jumatano 06 Novemba 2019. Benki ya Stanbic Tanzania leo imetangaza mkakati wakuzindua zaidi ya mashine 10 za kupokea miamala mikubwa ya fedha zijulikanazo kitaalamu kama ‘Bulk Note Acceptors (BNA)’. 

Stanbic inategemea kuzindua mashine hizo ifikapo mwakani. Kwa sasa, benki hiyo imesambaza mashine hizo katika matawi yake manne katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya,Arusha na Mwanza.
 
Mashine hizo za kisasa zinalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kuweka fedha kwa wateja wenyebiashara ndogo na za kati, pamoja na mashirika makubwa. Mashine za BNA zina uwezo wa kupokea hadi shilingi milioni mia moja na hamsini kwa muamala mmoja (yaani noti 15,000 kwa mkupuo). 

Hili ni ongezeko kubwa kutoka kiasi cha shilingi milioni mbili kinachoweza kupokelewa na mashine za awali
zilizopo katika matawi mengi zaidi kwa sasa.

Akizungumzia ongezeko la mashine za BNA, Bw. Brian Ndadzungira, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi
wa benki hiyo, alisema kuwa mashine hizo zitasaidia kuokoa muda wa wateja wenye biashara ndogo na kati ikiwa ni pamoja na kupunguza foleni katika matawi ya benki. “Usambazaji wa mashine hizi unalenga kurahisisha utendaji wa biashara ndogo na za kati na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi ili kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi,” alisema.

 Ndadzungira alibainisha kuwa benki hiyo inaendelea kufanya mapitio ya mifumo yake ya kiutendaji ili kusogeza huduma karibu zaidi kwa wateja, ikiwa ni jitihada za kuimarisha na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja wao. “Lengo letu la kila siku ni kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja wetu.

 Uzinduzi huu utawarahisishia upatikanaji wa huduma, jambo litakalowasaidia kutumia muda wao mwingi zaidi kuangazia maeneo mengine ya uzalishaji ya biashara zao,” alisema.

Dira ya Taifa ya mwaka 2025 imebainisha kuwa sekta inayosimamia biashara ndogo na za kati ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi. Kwa mujibu wa ripoti ya Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), sekta hiyo inajumuisha zaidi ya biashara milioni 3 ambazo huchangia asilimia 27 ya pato la taifa na kuajiri takribani watu milioni 5.2. Stanbic inaamini kuwa
uzinduzi wa huduma bora za kifedha utapelekea ukuaji zaidi wa sekta hiyo.
 
“Ni muhimu kubuni huduma hizi za kidijitali ili kusaidia ongezeko la biashara katika sekta binafsi. Jambo
litakalopelekea ongezeko la ajira, kipato na kujenga biashara endelevu,” alisema Ndadzungira.

No comments:

Post a Comment

Pages