HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 11, 2019

Polisi Arusha yawashikilia saba kwa ujangili wa twiga, meno ya tembo na bunduki mbili za kivita

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha (RPC), Jonathan Shana, akiwaonyesha waandishi wa habari meno ya tembo mawili, nyama ya twiga na bunduki mbili za kivita zilizokamatwa kwenye operesheni maalum ya kukabiliana na ujangili inayofanya na jeshi hilo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali. (Picha na Grace Macha).


NA GRACE MACHA, ARUSHA

 WATU saba wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za ujangili wakidaiwa kukutwa na meno ya tembo mawili na nyama ya twiga ambaye alikuwa wamemkatakata tayari kwa kuianika.

Aidha watu wengine wawili wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kutumia jina la gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, (BOT), Profesa, Florence Luoga kutapeli watu kupitia mtandao wa kijamii wa facebook.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, (RPC), Jonathan Shana, aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa watuhumiwa wa ujangili wamekamatwa kutokana na ushirikiano wa pamoja na Kikosi kazi cha Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,Kikosi  dhidi ya ujangili (KDU) Kanda ya
Kaskazini pamoja na kikosi kazi Taifa kinachopambana na ujangili Kanda
ya Ziwa.

Alisema watuhumiwa  wawili  wa ujangili , Nyamhanga Mwanga Mwita (19) na Chacha Marwa Mtocho (20) wote wakazi wa  Wilaya ya Serengeti Mkoani
Mara, walikamatwa wakiwa na  nyama ya Twiga, baada ya kumuua.

Alisema watuhumiwa hao wa walikamatwa Novemba 10, mwaka huu kwenye kijiji cha Oleng'usa ndani ya eneo la pori tengefu la Loliondo wilayani Ngorongoro.

"Watuhumiwa hao walikutwa wakiwa wanaendelea kuanika nyama hizo porini kwa ajili ya kuzisafirisha baada ya kuwa wamezikata vipande vipande," alisema kamanda Shana na kuongeza.

Pia wamekutwa na panga, sime mbili, tochi, kisu pamoja na nyaya za kutegea wanyama  zikiwa katika mafungunsaba,".

Kamanda Shana aliwataja watuhumiwa wengine wa ujangili aliodai kuwa walikutwa na na meno mawili ya tembo kuwa ni Thomas Sanjiro kiteo (29),Edward Sengeu Mollel (30),Emmanuel Meyani Sengeu (40),Lembris Lang’asan Meyan (45) wote wakazi wa Simanjiro, mkoani na Samweli Jacob Nassari (53) mkazi wa King’ori
Wilayani  Arumeru mkoani Arusha.

Alisema meno hayo yalipatikana Novemba 10 mwaka huu, majira ya saa 11:40 jioni maeneo ya Mbuyuni wilayani Arumeru, baada ya Polisi kupata taarifa za Kiintelijensia kuwa meno hayo yaliofichwa wilayani Simanjiro, yameletwa Arusha kwa ajili ya kuuza na watuhumiwa wapo
kwenye Pikipiki.

“Tuliweka mtego na tulikamata pikipiki mbili aina ya Kinglion yenye namba za usajili T 917 BUA na Sunlag yenye namba za usajili MC 819 ACD ambazo zilibeba meno hayo,” alisema kamanda Shana.

Pia jeshi hilo kwa kushirikiana na TANAPA, NCAA, KDU, kikosi kazi Taifa cha kinachopambana na ujangili Kanda ya Ziwa, walikamata bunduki mbili za kivita zikiwa na risasi 15.

Kamanda Shana alisema kuwa bunduki  hizo zilizokamatwa ni aina ya AK 47 yenye namba  174364 ikiwa na risasi  sita ndani ya Magazine pamoja na G3 yenye namba  A36011858 ikiwa na risasi tisa ndani ya magazine, ambapo bunduki zote zilikamatwa  karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Naani, tarafa ya Loliondo.

"Bunduki hizo zilipatikana baada ya majibizano ya risasi baina ya kikosi kazi hicho kabambe na majangili, mara baada ya kuona mashambulizi yamezidi . Majangili hao walizitelekeza silaha hizo na kukimbilia nchi jirani (Kenya)  alisema Kamanda Shana na kuongeza.

"Hata hivyo katika majibizano hayo jangili mmoja alijeruhiwa kwa risasi lakini alifanikiw akukimbia huku akivuja  damu  nyingi na sidhani kama amepona,”.

Wakati huo huo Kamanda Shana alisema kuwa jeshi hilo linawashikilia Juma Hussein Yahaya (33) mkazi wa Sakina  ambaye ni wakala wa kusajili laini za simu  na mwenzake Aman Gabriel Mbise (32) mkazi wa Sombetini kwa tuhuma za kutumia jina la Gavana wa Benki Kuu ya tanxsnia, (BOT), Prof.Florence Luoga katika mtandao wa Kijamii (Facebook) na kuwatapeli watu mbalimbali .

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 10, mwaka huu majira ya saa 11:40 baada ya jeshi hilo kupokea taarifa toka kwa Gavana kuhusiana na watu kutumia jina lake katika mtandao wa Facebook na kutapeli watu mbalimbali na kujenga nyumba eneo la Maji ya Chai Wilayani Arumeru.

"Tulipopata taarifa hizi tulianza upelelezi  kuhusiana na akaunti hiyo na tulibaini kuwa namba ya simu 0785349763 imesajiliwa kupitia akaunti hiyo,baada ya kuafuatilia namba hii tulibaini mtuhumiwa alisajili namba hiyo ya simu kwa kutumia hati ya kusafiria ya Norrish Andrew James raia wa Australia,"alisema kamanda Shana.

Alisema kuwa raia huyo wa Austaralia alifika nchini akitokea nchini Kenya na kufanya usajili wa namba ya simu kwa wakala aitwaye Juma Hussein ambaye alisajili laini za simu kwa kushirikiana na Aman Gabriel Mbise kwa kutumia hati hiyo hiyo kusajili namba ambayo walitumia kufanya uhalifu.

Kamanda Shana alisema baada ya kuwakamata watuhumiwa  hao na kufanya upekuzi kwa (Yahaya) alikutwa na laini mbalimbali  pamoja na simu sita na kukiri kuwa laini hiyo ya simu yake na aliiharibu baada ya kutapeli fedha na huwa kila anapotapeli anaharibu laini na kutafuta laini nyingine.

"Tumejipanga vizuri kuwakamata kwa urahisi kutokana na teknolojia tuliyonayo.pia tutawakamata wale wote waliopewa leseni/vibali vya kusajili laini za simu ambao wanatumia bibali hivyo kufanya uhalifu hasa wa kuwasajili watu kwa kutumia vitambulisho vya watu wengin,"alionya Kamanda Shana.

Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment

Pages